• HABARI MPYA

  Jumanne, Februari 26, 2019

  SIMBA SC YAENDELEZA WIMBI LA USHINDI LIGI KUU, YAICHAPA LIPULI FC 3-1 SAMORA

  Na Mwandishi Wetu, IRINGA
  SIMBA SC imeendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuwachapa wenyeji, Lipuli FC 3-1 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Samora mjini Iringa.
  Kwa ushindi huo, Simba SC inafikisha pointi 48 baada ya kucheza mechi 19, sasa ikizidiwa pointi mbili tu na Azam FC inayoshika nafasi ya pili kwa pointi zake 50 za mechi 25, wakati Yanga SC inaendelea kuongoza kwa pointi zake 61 za mechi 25. 
  Hadi mapumziko, Simba SC walikuwa mbele kwa 2-1 mabao yake yote yakifungwa na kiungo Mzambia, Clatous Chama huku bao pekee la Lipuli FC likifungwa na mshambuliaji wake Paul Nonga.  
  Chama aliifungia bao la kwanza Simba SC dakika ya tano akimalizia pasi nzuri ya beki wa kushoto, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ aliyenzishiwa mpira wa adhabu na mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi. 

  Mchezaji wa zamani wa Yanga, Paul Nonga akaifungia bao la kusawazisha Lipuli FC dakika ya 18 kwa shuti kali akiwa ndani ya boksi akimalizia pasi ya Daruwesh Saliboko.
  Chama akaifungia Simba SC bao la pili dakika ya 44 kwa shuti la moja kwa moja la mpira wa adhabu kutoka umbali wa mita 19 tu baada ya kiungo mwenzake, Muzamil Yassin kuangushwa.
  Kipindi cha pili mipango ya kocha Suleiman Matola iliharibika zaidi na Lipuli wakajikuta wakilainika zaidi mbele ya Simba SC.
  Mshambuliaji wa kimataifa wa Rwanda, Meddie Kagere mwenye asili ya Uganda akaifungia Simba SC bao la tatu dakika ya 58 akimalizia pasi ya kutanguliziwa na Chama kumtungua kwa mpira mrefu kipa wa Lipuli FC, Yusuph Mohammed.
  Lipuli iapata pigo dakika ya 68 baada ya beki wake wa kushoto, Paul Ngalema kutolewa kwa kadi nyekundu kufuatia kumpiga ngumi Nahodha wa Simba SC na mshambuliaji, John Raphael Bocco wakati wakigombea mpira.
  Simba SC iliendelea kupeleka mashambulizi langoni mwa Lipuli, lakini wakaishia kupoteza nafasi mbili nzuri walizotengeneza.
  Kikosi cha Lipuli FC kilikuwa; Yusuph Mohammed, William Lucian ‘Gallas’, Paul Ngalema, Ally Sonso, Haruna Shamte, Freddy Tangalu, Seif Karihe, Jimmy Shoji, Paul Nonga, Daruwesh Saliboko na Steven Mganga.
  Simba SC; Aishi Manula, Zana Coulibally, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Yusuph Mlipili, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Clatous Chama/Haruna Niyonzima dk84, Muzamil Yassin, John Bocco, Meddie Kagere/Adam Salamba dk90+1 na Emmanuel Okwi/Hassan Dilunga dk59.
  Mechi nyingine ya Ligi Kuu leo, Mtibwa Sugar wameutumia vyema Uwanja wa nyumbani, Manungu uliopo Turiani mkoani Morogoro kwa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Coastal Union.
  Mabao ya Mtibwa Sugar yamefungwa na Dickson Daudi dakika ya 40, Jaffar Kibaya dakika ya 55 na Riphat Msuya dakika ya 67, huku bao pekee la Coastal likifungwa na Ayoub Lyanga dakika ya 21.

  Kwa ushindi huo, Mtibwa Sugar inajiinua hadi nafasi ya 11 kutoka ya 17 kwenye Ligi Kuu ya timu 20, ikifikisha pointi 32 katika mechi ya 25, wakati Coastal Union inayobaki na pointi zake 34 za mechi 27 sasa, inabaki nafasi ya nane.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAENDELEZA WIMBI LA USHINDI LIGI KUU, YAICHAPA LIPULI FC 3-1 SAMORA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top