• HABARI MPYA

  Ijumaa, Februari 22, 2019

  KAGERE APIGA MBILI, BOCCO MOJA SIMBA SC YAWATANDIKA AZAM FC 3-1 TAIFA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC imeendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Azam FC 3-1 jioni ya leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Kwa ushindi huo, Wekundu wa Msimbazi wanafikisha pointi 45 baada ya kucheza mechi 18, ikiendelea kushika nafasi ya tatu, nyuma ya Azam FC inayobaki na pointi zake 50 baada ya kucheza mechi 25, huku Yanga SC ikiendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 61 za mechi 25 pia.
  Katika mchezo wa leo, mshambuliaji wa kimataifa wa Rwanda mwenye asili ya Uganda, Meddie Kagere alianza kuifungia Simba SC dakika ya tano tu kwa kichwa akimalizia mpira uliorudi baada ya kugonga mwamba kufuatia shuti la Nahodha na mshambuliaji mwenzake, John Raphael Bocco ‘Adebayor’.


  Meddie Kagere (kulia) akikimbia kushangilia leo baada ya kuifungia Simba SC bao la kwanza 

  Bocco naye akaiadhibu timu yake ya zamani kwa kuifungia Simba SC bao la pili dakika ya 39 kwa kichwa akimalizia krosi ya beki Zana Coulibally kutoka Burkina Faso aliyeanzishiwa kona fupi na mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi upande wa kulia. 
  Kagere tena dakika ya 77 akaifungia Simba SC bao la tatu kwa mguu wake wa kulia akimalizia pasi ya Mzambia, Clatous Chama aliyepokea pasi ya kiungo mwenzake, Muzamil Yassin ambaye ndiye kwanza alikuwa ameingia uwanjani kuchukua nafasi ya Okwi aliyeumia.
  Dakika ya 81 Frank Domayo aliyetokea benchi akaifungia Azam FC bao la kufutia machozi baada ya pasi ya mshambuliaji Mzimbabwe, Donald Ngoma kwa shuti kali lililogonga mwamba wa juu na kudondokea ndani ya mstari kabla ya mpira kurudi uwanjani, lakini refa Heri Sasii akawa makini na kuamuru uwekwe kati.
  Sasii akakataa bao lililofungwa na beki Aggrey Morris dakika ya 85 akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na beki Mzimbabwe, Bruce Kangwa kwa sababu alitumia mabega ya Kagere kuurukia mpira kupigwa kichwa kufunga.
  Kwa ujumla Simba SC inayofundishwa na kocha Mbelgiji, Patrick Aussems iliizidi uwezo Azam FC ya kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm leo na kuendelea kudhihirisha ubora wake unaowafanya wapewe nafasi kubwa ya kutetea ubingwa wao.
  Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Razack Abalora, Nico Wadada, Bruce Kangwa, Yakubu Mohammed, Aggrey Morris, Mudathir Yahya, Joseph Mahundi/Frank Domayo dk67, Tafadzwa Kutinyu/Donald Ngoma dk46, Obrey Chirwa, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Ramadhani Singano ‘Messi’/Enock Atta-Agyei dk46.
  Simba SC; Aishi Manula, Zana Coulibally, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Paul Bukaba, Pascal Wawa, James Kotei, Jonas Mkude, Clatous Chama/Rashid Juma dk90+2, John Bocco/Hassan Dilunga dk69, Meddie Kagere na Emmanuel Okwi/Muzamil Yassin dk74.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KAGERE APIGA MBILI, BOCCO MOJA SIMBA SC YAWATANDIKA AZAM FC 3-1 TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top