• HABARI MPYA

  Alhamisi, Februari 14, 2019

  AZAM YACHAPWA 1-0 NA PRISONS SOKOINE, YAFIKISHA MECHI TATU BILA USHINDI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TIMU ya Azam FC leo imekamilisha mechi tatu bila ushindi baada ya kuchapwa 1-0 na wenyeji, Tanania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
  Bao pekee la Tanzania Prisons limefungwa na Jumanne Elfadhili aliyemchambua kipa Benedict Haule kwa mkwaju wa penalti dakika ya 36 baada ya beki wa Azam FC, Mghana Yakubu Mohamed kuunawa mpira uliopigwa na Ezekia Mwashilimbi.
  Azam FC inabaki na pointi zake 48 baada ya kucheza mechi 22, ikiendelea kuzidiwa pointi tisa na vinara, Yanga SC ambao hata hivyo wamecheza mechi moja zaidi, wakati mabingwa watetezi, Simba SC ni wa tatu kwa pointi zao 36 za mechi 15.

  Mechi mbili zaidi za Ligi Kuu zinaendelea hivi sasa, Mwadui FC wakiikaribisha Coastal Union Uwanja wa Mwadui Complex, Kishapu mkoani Shinyanga na Biashara United wakiwa wenyeji wa Mtibwa Sugar Uwanja wa Karume mjini Musoma mkoani Mara.
  Ligi Kuu itaendelea kesho kwa mechi nne zaidi, Mbeya City wakiikaribisha Stand United ya Shinyanga Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, Ndanda FC wakiwa wenyeji wa Alliance FC ya Mwanza Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara, Mbao FC wakimenyana na Ruvu Shooting Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza na KMC na Kagera Sugar Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam.
  Jumamosi mabingwa watetezi, Simba SC watamenyana na mahasimu wao wa jadi, Yanga SC Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, wakati Jumapili Lipuli FC wataikaribisha Singida United Uwanja wa Samora mjini Iringa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AZAM YACHAPWA 1-0 NA PRISONS SOKOINE, YAFIKISHA MECHI TATU BILA USHINDI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top