• HABARI MPYA

  Ijumaa, Februari 15, 2019

  KABWILI YUKO TAYARI KUHIMILI MIKIKI YA PAMBANO LA WATANI?

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  WATANI wa jadi, Simba na Yanga wanakutana kesho katika mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Hiyo ni baada ya timu hizo kutoka sare ya bila kufungana katika mchezo wa kwanza uliofanyika Septemba 30, mwaka jana hapo hapo Uwanja wa Taifa.
  Siku hiyo, Yanga wakionekana kuwa na kikosi dhaifu kulinganisha na cha wapinzani wao, Simba walikwenda kucheza mchezo wa kujihami na kupata sare waliyoipigania.
  Hata hivyo, kipa Beno Kakolanya aliyejizolea sifa nyingi siku hiyo kwa kuokoa michomo mingi ya hatari hatakuwepo tena kesho kwenye lango la Yanga.

  Ramadhani Kabwili yuko tayari kuhimili mikiki ya pambano la watani wa jadi kesho?

  Beno alitofautiana na klabu kutokana na msimamo wake wa kudai haki zake kiasi cha kufikia kugoma na kocha Mwinyi Zahera, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) akaamua kumuondoa kwenye timu.
  Kipa chipukizi, Ramadhani Awam Kabwili ndiye anayeaminika zaidi ya Mkongo Klaus Kindoki kuelekea mechi ya kesho na bila shaka ndiye atakayeanza.   
  Baada ya kufanya vizuri akiwa na kikosi cha timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys kwenye fainali za Afrika (AFCON U17) nchini Gabon mwaka juzi, Kabwili aliyeibukia akademi ya Azam, akasajiliwa Yanga dirisha dogo msimu uliopita, Januari, 2018.
  Alisajiliwa kama kipa wa kikosi cha pili, U20, maarufu kama Yanga B ambaye alikuwa anakomazwa kikosi cha kwanza, wakati timu ya kwanza ikiwa na makipa, Mcameroon, Youthe Rostand na Kakolanya. 
  Lakini kutokana na matatizo ya Kakolanya na uongozi, akapandishwa mapema kikosi cha kwanza na kuanza kutumika tangu msimu uliopita akipewa hadi mechi za michuano ya Afrika.
  Rostand akaachwa na kusajiliwa Mkongo Kindoki msimu huu, lakini naye hajaweza kuwashawishi wana Yanga na kwa mwendelezo wa matatizo ya Kakolanya, imelazimika Kabwili awe kipa namba moja wa timu.  
  Hadi sasa, Kabwili amekwishaidakia Yanga jumla ya mechi 27 za mashindano yote, akiwa ameruhusu mabao 19 akiiwezesha timu kushinda mechi 18, sare tano na kufungwa nne. 
  Kabwili ambaye Desemba 11, mwaka jana amefikisha umri wa miaka 18 ndiye ‘Yanga One’ kwa sasa na ndiye anayepewa nafasi kubwa ya kuanza kesho.
  Historia yake inakumbushia kipa mwingine aliyeibukia Serengeti Boys, Peter Manyika ambaye akiwa ana umri wa miaka 18 alipewa nafasi ya kudaka kwenye mechi ya watani Oktoba 18, mwaka 2014 na akamaliza salama timu hizo zikitoka sare ya 0-0 Uwanja wa Taifa.
  Na wakati huo, kikosi cha Simba ndicho kilichoonekana dhaifu mbele ya Yanga, lakini Manyika aliyerithi majukumu ya baba yake, Manyika Peter kipa wa zamani wa kimataifa wa Tanzania pia, akajenga heshima kubwa siku hiyo.
  Je, Kabwili naye akiwa ana umri wa miaka 18 baada ya mechi 27 tu za kikosi cha kwanza, yuko tayari kuhimili mikiki ya pambano la watani wa jadi? Bila shaka hilo nio jambo la kusubiri na kuona.

  Ramadhani Kabwili ndiye ‘Yanga One’ kwa sasa anayepewa nafasi ya kuanza kesho dhidi ya Simba 

  REKODI YA RAMADHANI KABWILI YANGA SC

  1. Yanga 0-1 Ruvu Shooting (Alifungwa moja kirafiki -                Chamazi)
  2. Yanga 2-0 Mlandege (Hakufungwa Kirafiki Zanzibar)
  3. Yanga 1-0 Chipukizi (Aliingia kipindi cha pili kirafiki                  Zanzibar)
  4. Yanga 0-0 KMC (Hakufungwa Kirafiki Chamazi)
  5. Yanga 0-0 Rhino Rangers (Aliingia dk83 hakufungwa              Kirafiki Ally Hassan Mwinyi)
  6. Yanga 2-1 Mlandege (Alifungwa moja Kombe la                      Mapinduzi, Zanzibar)
  7. Yanga 2-0 Taifa Jang’ombe (Hakufungwa Kombe la                Mapinduzi, Zanzibar)
  8. Yanga SC 1-0 Zimamoto( Hakufungwa Kombe la                    Mapinduzi, Zanzibar)
  9. Yanga 2-0 Lipuli FC  (Hakufungwa, aliingia dk17 baada          ya Youthe Rostand kuumia, Samora, Iringa)
  10. Yanga 4-0 Njombe Mji FC  (Hakufungwa Ligi Kuu,                  Samora, Uhuru)
  11. Yanga 1-0 Saint Louis FC  (Hakufungwa Ligi ya                      Mabingwa, Taifa)
  12. Yanga 4-1 Maji Maji FC  (alifungwa moja kwa penalti,              Ligi Kuu, Taifa)
  13. Yanga 1-2 Township Rollers  (Alifungwa mbili Ligi ya               Mabingwa Taifa)
  14. Yanga 2-2 Ruvu Shooting FC (Alifungwa mbili Ligi Kuu          Taifa)
  15. Yanga 1-3 Azam FC (Alifungwa tatu Ligi Kuu Taifa)
  16. Yanga SC 2-0 Malindi FC (Hakufungwa Kirafiki                        Zanzibar)
  17. Yanga SC 1-2 Mwadui FC (Hakufungwa, aliingia kipindi          cha pili badala ya Kindoki Ligi Kuu Shinyanga)
  18. Yanga SC 2-1 Kagera Sugar (Alifungwa moja kwa                   penalti Ligi Kuu Bukoba)
  19. Yanga SC 3-1 Tanzania Prisons (Alifungwa moja kwa               penalti Ligi Kuu Sokoine)
  20. Yanga SC 2-1 Biashara United (Alifungwa moja Ligi                Kuu Taifa)
  21. Yanga SC 3-2 Ruvu Shooting (Alifungwa mbili Ligi Kuu          Taifa)
  22. Yanga SC 1-0 African Lyon (Hakufungwa, aliumia                    dakika ya 40 akaingia Kindoki Ligi Kuu Taifa)
  23. Yanga SC 2-1 Mbeya City (Alifungwa moja Ligi Kuu                Sokoine) 
  24. Yanga SC 2-2 (PENALTI 5-4) Biashara United                          (Alifungwa mbili na penalti 4 Kombe la TFF Taifa)
  25. Yanga SC 1-1 Coastal Union (Alifungwa moja Ligi Kuu             Mkwakwani)
  26. Yanga SC 0-0 Singida United (Hakufungwa Ligi Kuu               Namfua)
  27. Yanga SC 1-0 JKT Tanzania (Hakufungwa Ligi Kuu                  Mkwakwani)
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KABWILI YUKO TAYARI KUHIMILI MIKIKI YA PAMBANO LA WATANI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top