• HABARI MPYA

  Jumamosi, Februari 23, 2019

  AZAM FC YAWAFUKUZA PLUIJM NA MWAMBUSI BAADA YA KIPIGO CHA SIMBA JANA TAIFA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KLABU ya Azam FC imeachana na kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm pamoja na Msaidizi wake, mzawa Juma Mwambusi baada ya takriban miezi nane tangu waajiriwe.
  Wawili hao, ambao kwa pamoja wamewahi kuwa walimu wa klabu ya Yanga SC ya Dar es Salaam, walijiunga na timu mwanzoni mwa msimu, Pluijm akitokea Singida United na Mwambusi akiwa huru.
  Na pamoja na kuipa timu mataji mawili, Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame Agosti mwaka jana na Kombe la Mapinduzi Januari mwaka huu – lakini ajira zao zimesitishwa.

  Hans van der Pluijm (kushoto) na Msaidizi wake, Juma Mwambusi (katikati) wamefukuzwa 

  Ni maamuzi yanayotokana na mwenendo mbaya wa timu katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara, hadi sasa ikiwa imevuna pointi 50 katika mechi 25, ikizidiwa pointi 11 na vinara Yanga SC.
  Maamuzi haya yanakuja siku moja tu baada ya Azam FC kuchapwa mabao 3-1 na Simba SC katika mchezo wa Ligi Kuu Uwanja wa Taifa jana.
  Katika mchezo huo ambao makosa ya safu ya ulinzi yaliigharimu timu hiyo, mabao ya Simba SC yalifungwa na Meddie Kagere mawili na Nahodha wake, John Bocco moja wakati la Azam FC lilifungwa na kiungo Frank Domayo.    
  Kwa sasa timu itakuwa chini ya kocha wa kikosi cha timu ya vijana, Iddi Nassor Cheche wakati zoezi la kumpata kocha mpya likiendelea.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AZAM FC YAWAFUKUZA PLUIJM NA MWAMBUSI BAADA YA KIPIGO CHA SIMBA JANA TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top