• HABARI MPYA

  Jumamosi, Februari 16, 2019

  SIMBA SC YAWAZIMA WATANI WA TAIFA, YAWACHAPA YANGA 1-0 BAO LA KEGERE TAIFA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  BAO pekee la mshambuliaji Mnyarwanda mwenye asili ya Uganda, Mohammed ‘Meddie’ Kagere limetosha kuipa Simba SC ushindi wa 1-0 dhidi ya mahasimu wa jadi, Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Ushindi huo unawafanya Simba SC wafikishe pointi 39 baada ya kucheza mechi 16, ikipanda hadi nafasi ya tatu kutoka ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu, sasa ikizidiwa pointi 10 na Azam FC na 19 na Yanga SC wanaoongoza, baada ya wote kucheza mechi 23.  
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Hance Mabena aliyesaidiwa na washika vibendera Mohammed Mkono, wote wa Tanga na Kassim Mpanga wa Dar es Salaam, Kagere alifunga bao hilo dakika ya 72 kwa kichwa akiruka katikati ya mabeki wa Yanga Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na Paulo Godfrey ‘Boxer’ kuunganisha krosi ya Nahodha John Raphael Bocco.

  Pamoja na kuanza na washambuliaji watatu, Mrundi Amissi Tambwe, Heritier Makambo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na mzawa, Ibrahim Ajibu, lakini Yanga kwa mara nyingine leo imecheza kwa kujilinda zaidi, ikishambulia kuwa kushitukiza.
  Angalau leo ilitengeneza mashambulizi ya nguvu tofauti na Septemba 30 ikifanikiwa kupata sare ya 0-0 na Simba, lakini mshambuliaji wake Makambo hakuwa na bahati kutokana na kupoteza nafasi mbili za wazi, moja kila kipindi.  
  Dakika ya 39 Makambo aliye katika msimu wake wa kwanza Yanga SC, aliunganishia nje kwa kichwa krosi nzuri ya Ibrahim Ajibu kutoka upande wa kulia ambayo iliwapita mabeki wa Simba na kipa wao, Aishi Manula.
  Na Amissi Tambwe akaonyeshwa kadi ya njano dakika ya 45 kwa kujaribu kuucheza mpira kwa mkopo akiwa kwenye boksi la Simba. 
  Dakika ya 87 Makambo tena akapatwa na kigugumizi cha miguu akiwa amebaki na kipa Aishi Manula baada ya kupenyezewa pasi nzuri na Mrisho Ngassa hadi kipa huyo akapangua kabla ya beki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kuondoa kwenye hatari.
  Lakini ni Simba SC iliyotawala zaidi mchezo kwa ujumla, hususan baada ya mabadiliko ya mapema kipindi cha pili, Hassan Dilunga ‘HD’ akiingizwa kwenda kuchukua nafasi ya kiungo Mzambia, Clatous Chama.
  Dakika ya 58 Okwi alipiga shuti kali likagonga mwamba wa juu na kwenda nje, kabla ya Jonas Mkude naye kufumua shuti dakika moja baadaye likaenda mikononi mwa kipa chipukizi wa Yanga, Ramadhani Awam Kabwili.
  Shambulizi kali zaidi la Simba langoni mwa Yanga lilikuwa dakika ya 65 wakati Bocco alipounganisha kwa kichwa krosi ya Tshabalala, lakini Abdallah Shaibu ‘Ninja’ akaokoa, Kagere akajibu kwa shuti na beki huyo akaokoa tena katika mstari.
  Kwa ujumla Simba ilipiga mashuti matatu yaliyolenga lango dhidi ya moja la Yanga, 11 yaliyokwenda nje dhidi ya matano huku ikipiga kona nne dhidi ya mbili wapinzani wao.
  Mwishoni mwa mchezo mchezo kiungo wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’ alimsukuma Kagere wakati anatoka taratibu baada ya kufanyiwa mabadiliko kumpisha Mnyarwanda mwenzake, Haruna Niyonzima.
  Refa alimuonya kwa kadi ya njano Kagere kwa kujichelewesha kutoka na akawa mchezaji wa tatu wa Simba kuonyeshwa kadi hiyo baada ya beki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Emmanuel Okwi.
  Mabena pia aliwaonyesha kadi za njano wachezaji wanne wa Yanga, Gardiel Michael, Kelvin Yondan, Feisal Salum na Tambwe.    
  Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ramadhani Kabwili, Paulo Godfrey ‘Boxer’, Gardiel Michael/Matheo Anthony dk77, Andrew Vincent ‘Dante’, Kelvin Yondan, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Papy Kabamba Tshishimbi, Heritier Makambo, Amissi Tambwe/Mrisho Ngassa dk46 na Ibrahim Ajibu/Mohammed Issa ‘Banka’ dk61.
  Simba SC; Aishi Manula, Zana Coulibaly, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Juuko Murshid, Serge Wawa, James Kotei, Clatous Chama/Hassan Dilunga dk46, Jonas Mkude, John Bocco, Meddie Kagere/ Haruna Niyonzima dk90+2 na Emmanuel Okwi/Emmanuel Okwi dk86.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAWAZIMA WATANI WA TAIFA, YAWACHAPA YANGA 1-0 BAO LA KEGERE TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top