• HABARI MPYA

  Ijumaa, Februari 15, 2019

  KAMATI YA NIDHAMU YARUHUSU NINJA KUICHEZEA YANGA KESHO DHIDI YA MAHASIMU, SIMBA SC

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KAMATI ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imeridhia ombi la klabu ya Yanga kuahirisha kusikiliza shauri dhidi ya beki wake, Abdallah Hajji Shaibu ‘Ninja’ kwa sababu alipata wito wa kuhudhuria kikao akiwa nje ya Dar es Salaam.
  Uamuzi huo unamaanisha Ninja atakuwa huru kuichezea klabu yake, Yanga SC katika mechi ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya mahasimu wa jadi, Simba SC Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Taarifa ya Afisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Cliford Mario Ndimbo kwa Vyombo vya Habari leo imesema kwamba katika kikao chake Februari 9, mwaka huu chini ya Mwenyekiti wake, Wakili Kiomoni Kibamba, Kamati imekubali ombi la Yanga na shauri hilo litasikilizwa katika kikao kijacho.

  Abdallah Shaibu ‘Ninja’ (kushoto) yuko huru kuichezea Yanga SC dhidi Simba SC kesho Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam

  Ikumbukwe, Bodi ya Ligi imemlalamikia mchezaji huyo kwa kumpiga kiwiko mchezaji wa Coastal Union katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara baina ya timu hizo Februari 3, 2019 kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
  Na Ndimbo amesema kwamba Kamati imeonya haitapokea udhuru mwingine wowote isipokuwa kama atakuwa na majukumu katika timu ya Taifa.
  Pamoja na suala la Ninja, katika kikao hicho Kamati ilipitia mashauri mengine 14 yaliyowasilishwa mbele yake na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania na kuchukua hatua tofauti.
  Wakati huo huo: Mtunza Vifaa (Kit Man) wa Ruvu Shooting, Bw. Augustine Palangwa amepewa Onyo kwa kosa la kuzungumza na mwamuzi bila utaratibu katika mechi dhidi ya Yanga iliyofanyika Desemba 16, 2018 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
  Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Ibara ya 10(a) ya Kanuni za Nidhamu za TFF na kwa kosa la kutoa lugha ya matusi dhidi ya mwamuzi, Kamati haikumpata na hatia kwa sababu baada ya kupitia maelezo ya mlalamikaji na ripoti zote, kosa hilo limeshindwa kuthibitishwa kwa sababu ripoti za kamishna na mwamuzi zimetofautiana kuhusu tukio hilo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KAMATI YA NIDHAMU YARUHUSU NINJA KUICHEZEA YANGA KESHO DHIDI YA MAHASIMU, SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top