• HABARI MPYA

  Jumamosi, Februari 23, 2019

  SINGIDA UNITED YATINGA ROBO FAINALI ASFC BAADA YA KUIPIGA COASTAL UNION 1-0

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  BAO la kujifunga la Kennedy Kipepe dakika ya tano limeipa ushindi wa 1-0 Singida United dhidi ya Coastal Union ya Tanga usiku wa leo katika mchezo wa Hatua ya 16 Bora ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) Uwanja wa Azam Complex, Chamazi mjini Dar es Salaam.
  Kwa ushindi huo, Singida United inakwenda Robo Fainali ya michuano hiyo kwa mara ya pili mfululizo, ikiungana na Kagera Sugar, KMC na Lipuli FC zilioshinda mechi zao za mapema leo na kusonga mbele. 
  KMC imeitoa Mtibwa Sugar waliokuwa mabingwa baada ya kuwafunga kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90 Uwanja wa Azam Complex, Chamazi mjini Dar es Salaam.
  Refa wa kike, Jeonesiya Rukyaa alisukumana kwa kifua na kipa wa Mtibwa Sugar, Benedictor Tinocco baada ya mchezaji huyo kukasirishwa na uamuzi wa kurudiwa kwa penalti aliyoiokoa iliyopigwa na mlinda mlango mwenzake, Mrundi Jonathan Nahimana ambaye aliporudia alipofunga.  
  Waliofunga penalti za KMC ni Yussuf Ndikumana, Emmanuel Mvuyekure, kipa Jonathan Nahimana wote Warundi na Salum Chukwu, wakati Ismail Gambo yake ilipanguliwa na kipa wa Mtibwa Sugar, Benedictor Tinocco.
  Waliofunga penalti za Mtibwa Sugar, timu kutoka Manungu, Turiani mkoani Morogoro ni Salum Kihimbwa, Henry Joseph na Hassan Isihaka, wakati za Nassor Kapama na Shaaban Nditi zilipanguliwa na kipa Mrundi wa timu ya Manispaa ya Kinondoni.  
  Mtibwa Sugar inaingia kwenye orodha ya mabingwa wengine wa michuano hiyo walioshindwa kufika fainali, ambao ni Yanga mwaka juzi na Simba SC mwaka jana. Naye kocha Mrundi Etienne Ndayiragijje ameweka rekodi ya kuzifua ubingwa timu mbili, baada ya kuwatoa Yanga SC katika Nusu Fainali pia mwaka juzi akiwa na Mbao FC mjini Mwanza.  
  Mechi nyingine za hatua ya 16 Bora ya michuano hiyo leo, Kagera Sugar imeifunga 2-1 Boma FC ya Mbeya Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba na Lipuli FC imeichapa 3-1 Dodoma FC Uwanja wa Samora mjini Iringa.
  Michuano hiyo itaendelea kesho kwa mechi tatu, Namungo FC ikimenyana na Yanga SC Uwanja wa Kassim Majaliwa mjini Ruangwa mkoani Lindi, Alliance FC na Dar City FC Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza na African Lyon FC dhidi ya Mbeya City FC Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam, mechi zote zikianza Saa 10:00 jioni.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SINGIDA UNITED YATINGA ROBO FAINALI ASFC BAADA YA KUIPIGA COASTAL UNION 1-0 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top