• HABARI MPYA

  Ijumaa, Februari 15, 2019

  KAJUMULO AWAAMBIA CHIPUKIZI WASIFURAHIE SIMBA NA YANGA KUFANYA VIBAYA MICHUANO YA KIMATAIFA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MKUFUNZI wa kimataifa anayetambulika na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Alex Kajumulo amewaambia wachezaji chipukizi wasifurahie kuona Simba au Yanga zinapata matokeo mabaya katika mashindano mbalimbali ya kimataifa wanayoshiriki.
  Kajumulo alisema yao jana asubuhi wakati alipowatembelea wachezaji wa Kituo cha Michezo cha Mwenge (MSA) kilichoko jijini Dar es Salaam.
  Aliwaambia nyota hao kuwa wanatakiwa kuumia wanapoona timu hizo kongwe nchini zinafungwa kwa sababu matokeo hayo mabaya yanapunguza nafasi za wachezaji chipukizi kusajiliwa na timu za Ulaya.
  "Napenda kuwaambia kuwa hampaswi kufurahia ukiona Yanga au Simba inafungwa, hao wanapokuwa huko kwenye mashindano wanatangaza jina la Tanzania, wanapofungwa, hiyo inapunguza nafasi kwenu kupata timu, inabidi msikie machungu, hakuna anayeweza kuacha mchezaji kutoka nchi ambayo klabu zake zinapata matokeo mazuri," alisema Kajumulo.
  Alex Kajumulo (wa pili kushoto) akizungumza na wachezaji wa Kituo cha Michezo cha Mwenge (MSA), Dar es Salaam 

  Aliongeza kwa kuwaambia chipukizi hao kufanya mazoezi zaidi ya binafsi na kuacha kusubiri programu zinazoandaliwa na makocha wao pekee.
  Pia nyota huyo aliwaambia wachezaji hao chipukizi ambao wanaanzia umri wa miaka 14 hadi 23 kuwa wanatakiwa vile vile kujifunza lugha ya Kiingereza kwa ajili ya kurahisisha mawasiliano kati yao na wakufunzi ambao wanaweza kukutana nao katika siku za usoni.
  "Lugha ni kitu kimojawapo kilichomwangusha Ngasa (Mrisho), kama hujui Kiingereza inabidi uwe na kitu cha ziada kuwafanya wakusajili, labda uwe kama Messi (Lionel), ambaye wanaweza kukuwekea mkalimani, pia usisubiri mazoezi ya kocha, unatakiwa ufike mapema na kuanza kujifua mwenyewe, hii itakusaidia," Kajumulo alisema.
  Aliwataka wachezaji hao pia kutokata tamaa wakati wanahitaji kutimiza ndoto zao.
  "Mimi nilipokwenda Ufaransa, niliwahi kukaa benchi miezi sita, lakini sikukata tamaa, pia nilipenda kukaa karibu na kocha ili kusikia namna anavyoelekeza na anavyofanya mabadiliko, hii ilinijenga sana na siku nilipopata nafasi nilionyesha kiwango changu,...mpira sasa ni biashara, mnatakiwa mpambane," aliongeza mdau huyo.
  Ramadhan Kagua, mmoja wa wajumbe wa bodi ya MSA alimshukuru Kajumulo kwa kutembelea kituo hicho na kumtaka aendelee kuwasiliana nao kwa malengo ya kutoa ushauri na misaada ya aina mbalimbali.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KAJUMULO AWAAMBIA CHIPUKIZI WASIFURAHIE SIMBA NA YANGA KUFANYA VIBAYA MICHUANO YA KIMATAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top