• HABARI MPYA

  Alhamisi, Februari 14, 2019

  ULIMWENGU: TIMU YOYOTE INAWEZA KUFUZU ROBO FAINALI KUNDI D LIGI YA MABINGWA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Thomas Emmanuel Ulimwengu amesema kwamba timu zozote mbili kati ya nne za Kundi D zinaweza kufuzu Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka huu.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo kwa simu kutoka Bechar, Ulimwengu anayechezea JS Saoura ya Algeria, iliyopangwa kundi moja na Simba SC ya Tanzania, Al Ahly ya Misri na AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) amesema kundi hilo limekuwa gumu sasa.
  Ulimwengu amesema baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya AS Vita usiku wa Jumanne Uwanja wa Agosti 20, 1955 mjini Bechar nchini Algeria, JS Saoura imefufua matumaini ya kwenda Robo Fainali sawa na Simba SC iliyoifunga Al Ahly 1-0 pia mapema siku hiyo. 

  Thomas Ulimwengu amesema timu yoyote Kundi D inaweza kufuzu Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka huu

  “Kundi letu limekuwa gumu sasa, timu yoyote inaweza kufuzu, hata sisi (JS Saoura) na Simba SC ambao awali tulichukuliwa hatuna nafasi kabisa, tunaelekea kwenye mechi mbili za mwisho tukiwa na nafasi,”amesema Ulimwengu aliyejiounga na timu hiyo Januari.
  Baada ya ushindi uliotokana na bao pekee la kiungo Muagleria Ziri Hammar dakika ya 78 akitumia vyema kabisa makosa ya walinzi wa AS Vita, JS Saoura imepanda hadi nafasi ya tatu ikifikisha pointi tano, nyuma ya Simba yenye pointi sita na Al Ahly saba.
  Ikumbukwe mechi zilizopita JS Saoura ilifungwa 3-0 na Simba mjini Dar es Salaam, ikatoa sare za 1-1 na Al Ahly mjini Bechar na 2-2 na AS Vita mjini Kinshasa.
  Mechi zijazo, Saoura ataikaribisha Simba SC mjini Bechar na AS Vita wataikaribisha Al Ahly mjini Kinshasa Jumamosi ya Machi 9.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: ULIMWENGU: TIMU YOYOTE INAWEZA KUFUZU ROBO FAINALI KUNDI D LIGI YA MABINGWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top