• HABARI MPYA

  Alhamisi, Februari 21, 2019

  IMANI ZA KISHIRIKINA NA HARAKATI ZA KUHARIBU SOKA YA TANZANIA

  Na Frederick Daudi, DAR ES SALAAM
  SIKU moja timu ya mtaani kwetu ikiwa na kibarua kigumu dhidi ya wapinzani wetu wa jadi, tukaambiwa tupakwe dawa fulani ndipo tushinde. Nikauliza swali, "tunatumiaje uchawi halafu tukifika uwanjani tunajikusanya tunamwomba Mungu?" Jibu nililopata ni kwamba, hata Mungu anasaidiwa. Yaani, ukichanganya Mungu na ushirikina ndipo unafanikiwa.
  Nilipigwa na butwaa kwani nilikuwa nafahamu vizuri kabisa kwamba hakuna uhusiano wowote kati ya nuru na giza ( Mungu na Shetani). Licha ya baadhi ya wachezaji wetu kutii masharti yale, tulipoteza mechi ile.
  Hivyo ndivyo mambo yalivyo kwenye soka letu. Si ligi ya kuku wala ya kondoo. Sio ndondo wala kombe la ng'ombe, siyo ligi daraja la kwanza wala ligi kuu; kote mambo ni yaleyale.

  Miongoni mwa vitu ambavyo  vimekuwa vikilitia doa na kulipaka matope soka letu ni ushirikina. Pamoja na TFF kukemea vitendo hivi na hata kutoa adhabu kwa wahusika, bado wenye imani zao wanazidi kufanya mazingaombwe hayo.
  Achana na huko mtaani. Kinachoniuma zaidi ni kuona vitendo hivi vinafanyika kwenye ligi kuu. Ligi ambayo tunatarajia bingwa wake akaiwakilishe nchi kwenye michuano ya Afrika na hatimaye kwenye michuano ya dunia.
  Ligi ambayo tunatarajia iwatoe wachezaji watakaocheza ligi kubwa duniani kama Uingereza na Hispania. Au wewe mchezaji unadhani utachukua tuzo ya mchezaji bora wa Afrika au dunia kwa kutegemea ndumba?
  Hii ni aibu kubwa na inatia kinyaa. Yaani hadi hizi timu kongwe za Kariakoo zinatumia ukongwe wao kuudhihirishia umma wa Watanzania uhenga wao kwenye uchawi? Kwani hamuoni kwamba tangu muanzishwe zaidi ya miaka 80 iliyopita uchawi haujawahi kuwasaidia? 
  Kama ni kuroga mmeroga mara ngapi? Kama ni waganga mmebadilisha kiasi gani? Mbona bado hata kufuzu tu hatua ya makundi ya kombe la CAF imekuwa mtihani?
  Vitendo vya mashabiki kutaka kutoana roho kisa uchawi vimekithiri. Vitendo vya wachezaji kuchimba golini ili kuondoa dawa vinashiria ushamba na uzamani.
  Pamoja na mambo mengine, ndumba inachangia kwa kiasi kikubwa sana kuturudisha nyuma. Wachezaji, mabenchi ya ufundi na mashabiki wamejenga imani yao kwamba bila uchawi ushindi haupo. Cha ajabu timu zinaishia hapahapa Tanzania.
  Badala ya kutegemea uwekezaji na mifumo ya kisasa ya uendeshaji wa soka, wanajenga imani yao juu ya madude yasiyoonekana. Au mnadhani Barcelona, Real Madrid na Manchester united zimefanikiwa kwa sababu ya uchawi? Kwanini Chelsea na Man city hazikupata mafanikio makubwa  kama waliyonayo sasa kabla ya uwekezaji mkubwa wa Abramovich na Shekh Mansour? 
  Inasikitisha sana kuona kwamba wakati timu zingine zikifanya jitihada za dhati kupanda chati, timu za Tanzania zinafanya jitihada za kumwaga damu magetini, kuchimba vitu uwanjani na kupita kwenye milango isiyo halali kisa wanakwepa dawa. Pointi tatu hazitafutwi hivyo jamani.
  Kuna watu nasikia wanaitwa wazee. Mimi nilitarajia kwamba wangekuwa na ushauri wa kisasa wa kuzisaidia timu zetu kutokana na uzoefu wao. Kumbe wana ajenda ya siri?
  Tangu niumbwe, nianze kucheza mpira na kuangalia mechi kadha wa kadha za mtaani na ligi kuu,  sijawahi kuona mchango chanya wa ushirikina kwenye upatikanaji wa ushindi. Ndio, uchawi hausadii chochote kwenye mpira. Kama uchawi ungekuwa unasadia,  timu za vijijini kwetu huko kama Nyarombo, Omoche, Siko au Nyabikondo zingekuwa si tu zimeshachukua ligi kuu Tanzania, bali hata klabu bingwa duniani.
  Laiti tungelitambua kwamba ushirikina hausaidii kwenye soka, Taifa Stars isingelikaa miaka 39 bila kucheza AFCON. Simba na Yanga zisingelikuwa zinatolewa kila mwaka kwenye hatua za awali. Tubadilike jamani. Mpira unachezwa uwanjani, hauchezwi kwa sangoma.
  (Frederick Daudi ni mwanafunzi wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam kwenye Shule ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC). Anapatikana kwa namba 0742164329 na e-mail defederico131@gmail.com).
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: IMANI ZA KISHIRIKINA NA HARAKATI ZA KUHARIBU SOKA YA TANZANIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top