• HABARI MPYA

  Jumapili, Februari 17, 2019

  SAMATTA AFIKISHA MABAO 20 MSIMU HUU LIGI YA UBELGIJI GENK IKICHAPWA 3-1 UGENINI

  Na Mwandishi Wetu, BRUGGE 
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta usiku huu amefunga bao pekee la timu yake KRC Genk ikichapwa mabao 3-1 na wenyeji, Club Brugge katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji Uwanja wa Jan Breydel mjini Brugge.
  Samatta alifunga bao hilo dakika ya 77 akimalizia pasi ya Ruslan Malinovskiy, baada ya Club Brugge kutangulia kwa mabao ya Clinton Mata dakika ya 21 na Siebe Schrijvers dakika ya 37.  
  Hata hivyo, wakati Genk ikihangaika kusaka bao la kusawazisha, ikajikuta inapachikwa bao la tatu dakika ya 78, mfungaji Ruud Vormer aliyemalizia kazi nzuri ya Krepin Diatta.
  Pamoja na kufungwa, Genk inaendelea kuongoza Ligi hiyo kwa pointi zake 57, ikifuatiwa na Club Brugge yenye pointi 49 sasa, Standard Liege pointi 46 na Antwerp pointi 45 baada ya wote kucheza mechi 26.
  Mbwana Samatta akinyoosha kidole juu baada ya kuifungia Genk bao pekee leo  ikichapwa mabao 3-1 na Club Brugge
  Mbwana Samatta akimtoka mchezajni wa Club Brugge kwenye mchezo wa leo

  Leo Samatta amefunga bao la 20 la msimu katika ligi hiyo, akiendelea kuongoza chati ya wafungaji, akifuatiwa na Mtunisia Hamdi Harbaoui wa Zulte-Waregem mwenye mabao 14 na Mbelgiji mzaliwa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Landry Nany Dimata wa Anderlecht.
  Kwa Samatta mwenye umri wa miaka 26, leo amefikisha mabao 59 ya kuifungia Genk katika jumla ya mechi 143 za mashindano yote tangu amejiunga nayo Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
  Katika ligi ya Ubelgiji pekee amefikisha mabao 44 kwenye mechi 110, wakati mabao mengine 14 amefunga katika mechi 23 za Europa League na mawili kwenye tisa za Kombe la Ubelgiji.
  Kikosi cha Club Bruges leo kilikuwa: Horvath, Poulain, Denswil, Mechele, Mata/Amrabat dk28, Diatta, Schrijvers/Nakamba dk83, Vanaken, Vormer, Zits na Wesley/Openda dk87.
  KRC Genk: Vukovic, Maehle, Aidoo, Dewaest, Uronen, Heynen/De Norre dk94, Malinovskyi, Ingvartsen/Pozuelo dk45, Paintsil/Gano dk45, Trossard na Samatta.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SAMATTA AFIKISHA MABAO 20 MSIMU HUU LIGI YA UBELGIJI GENK IKICHAPWA 3-1 UGENINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top