• HABARI MPYA

  Alhamisi, Februari 14, 2019

  BIASHARA UNITED YAICHAPA MTIBWA SUGAR 2-1, MWADUI FC YAIPIGA COASTAL UNION

  Na Mwandishi Wetu, MUSOMA
  TIMU ya Biashara United imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Karume mjini Musoma mkoani Mara.
  Mabao ya Biashara United leo yamefungwa na George Makang’a dakika ya 39 na Innocent Edwin dakika ya 80, wakati bao pekee la Mtibwa Sugar limefungwa na mtokea benchi Riphat Khamis dakika ya 64.
  Kwa ushindi huo, Biashara United inayofundishwa na beki wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Amri Said ‘Stam’ inafikisha pointi 23 baada ya kucheza mechi 27 na kupanda kwa nafasi moja hadi ya 19 kwenye ligi ya timu 20, ikiishushia mkiani African Lyon yenye pointi 20 za mechi 24.
  Mtibwa Sugar, mabingwa wa Ligi Kuu mara mbili mfululizo 1999 na 2000 inabaki na pointi zake 29 baada ya kucheza mechi 23, ikiendelea kukamata nafasi ya 11.
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Mwadui FC imeibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Coastal Union ya Tanga Uwanja wa Mwadui Complex, Kishapu mkoani Shinyanga mabao yake yakifungwa na Wallece Kiango dakika ya 65 na Salim Aiyee dakika ya 79 dhidi ya lile la Ayoub Lyanga dakika ya 75.
  Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, bao pekee la Jumanne Elfadhili dakika ya 36 limeipa Tanzania Prisons ushindi wa 1-0 dhidi ya Azam FC.
  Azam FC inabaki na pointi zake 48 baada ya kucheza mechi 22, ikiendelea kuzidiwa pointi tisa na vinara, Yanga SC ambao hata hivyo wamecheza mechi moja zaidi, wakati mabingwa watetezi, Simba SC ni wa tatu kwa pointi zao 36 za mechi 15.
  Ligi Kuu itaendelea kesho kwa mechi nne zaidi, Mbeya City wakiikaribisha Stand United ya Shinyanga Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, Ndanda FC wakiwa wenyeji wa Alliance FC ya Mwanza Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara, Mbao FC wakimenyana na Ruvu Shooting Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza na KMC na Kagera Sugar Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam.
  Jumamosi mabingwa watetezi, Simba SC watamenyana na mahasimu wao wa jadi, Yanga SC Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, wakati Jumapili Lipuli FC wataikaribisha Singida United Uwanja wa Samora mjini Iringa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: BIASHARA UNITED YAICHAPA MTIBWA SUGAR 2-1, MWADUI FC YAIPIGA COASTAL UNION Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top