• HABARI MPYA

    Monday, January 08, 2018

    CHAMA KUZIKWA KESHO MCHANA MAKABURI YA KISUTU

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MWILI wa beki wa zamani wa kimataifa nchini, Athumani Juma ‘Chama’ utahifadhiwa kesho mchana katika makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam baada ya sala ya Adhuhuri.
    Katibu Mkuu wa Yanga SC, Charles Boniface Mkwasa amesema leo mjini Dar es Salaam kwamba msiba wa Chama aliyefariki dunia usiku wa kuamkia leo katika hospitali ya Muhimbili mjini Dar es Salaam upo nyumbani kwake, Yombo Mwisho.
    Mkwasa amesema kwamba mwili wa marehemu utafanyiwa sala katika msikiti wa Manyema, Kariakoo kabla ya kwenda kuhifadhiwa kwenye makaburi ya Kisutu.

    Athumani Juma 'Chama' (katikati) akiwa na wachezaji chipukizi wa Yanga mwaka 1986, Athumani China (kulia) na Abubakar Salum 'Sure Boy' (kushoto)

    "Tunawaomba wana Yanga wote tuungane kwa pamoja na familia ya marehemu katika kipindi hiki kigumu. Chama alikuwa mchezaji mahiri wa Yanga na alifanya mengi mazuri kwa timu na taifa enzi za uhai wake,”amesema Mkwasa.
    Naye Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia amesema amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Chama.
    “Ni masikitiko makubwa kumpoteza Chama ambaye alilitumikia taifa, naungana kumuombea marehemu na ninatoa pole kwa familia yake, wana familia ya mpira wa miguu, ndugu na jamaa zake wa karibu pamoja na marafiki,”amesema Karia.
    Kisoka, Chama aliibukia Pamba FC ya Mwanza mwaka 1977 alikozaliwa na kukulia kabla ya kujiunga na Yanga SC 1981 na aliocheza nao wakati huo ni akina Joseph Fungo, Yussuf Ismail Bana, Ahmed Amasha ‘Mathematician’, Isihaka Hassan Chukwu, Juma Mukambi ‘Jenerali’, Hussein Iddi, Charles Boniface Mkwasa, Abeid Mziba ‘JJ Masiga’, Elisha John, Ali Mchumila, Makumbi Juma ‘Homa ya jiji’, Omar Hussein ‘Keegan’, Juma Kampala na wengineo.
    Chama pia alikuwa akijulikana kwa jina lingine la utani, Jogoo ambalo alipewa mwaka 1981 kwenye michuano ya CECAFA Challenge nchini Kenya kutokana na mchezaji mmoja wa Harambee Stars, Sammy Onyango ‘Jogoo’. 
    Chama alistaafu soka mwaka 1990 na kujikita kwenye biashara zake ndogo ndogo kabla ya kuanza kusumbuliwa na maradhi mwaka 2014 na kujikuta anashindwa kufanya shughuli zake hadi umauti wake.
    Mungu ampumzishe kwa amani marehemu. Amin.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: CHAMA KUZIKWA KESHO MCHANA MAKABURI YA KISUTU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top