TIMU ya Singida Black Stars imeibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Airtel Mwigulu mjini Singida.
Mabao ya Singida Black Stars yamefungwa na beki wa kulia Muivory Coast, Ande Koffi Habib Cirille dakika ya 16, mshambuliaji Mkongo, Malanga Horso Mwaku dakika ya 17, kiungo Mganda Khalid Aucho dakika ya 82 kwa penalty na winga Mrundi, Mossi Nduwumwe dakika ya 88 baada ya kiungo Morice Ugochukwu Chukwu kujifunga dakika ya tatu kuipatia Mbeya City bao la kuongoza.
Kwa ushindi huo, Singida Black Stars imefikisha pointi 41 ingawa inabaki nafasi ya nne, wakati Mbeya City inabaki na pointi zake 22 nafasi ya 14 baada ya timu hizo mbili kucheza mechi 25 kwenye ligi ya timu 16.
Ikumbukwe mwisho wa msimu timu mbili zitashuka Daraja moja kwa moja, wakati nyingine mbili zitakazomaliza nafasi ya 14 na 13 zitamenyana baina yao kwa mechi mbili za nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla atasalia Ligi Kuu.
Timu itakayofungwa itakwenda kumenyana na timu kutoka Ligi ya Championship katika mechi nyingine mbili za mchujo nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla ndiye atacheza Ligi Kuu msimu ujao.



.png)
0 comments:
Post a Comment