• HABARI MPYA

    Wednesday, December 07, 2016

    MAMELODI SUNDOWNS WAHAMISHIA UBABE WAO DUNIANI

    TIMU ya Mamelodi Sundowns imehamishia cheche zake katika Klabu Bingwa ya Dunia baada ya kuwa klabu ya pili ya Afrika Kusini kutwaa taji Ligi ya Mabingwa Afrika ndani ya miaka 21 Oktoba mwaka huu.
    Timu hiyo yenye maskani yake Pretoria ilikuwa imekwishatolewa katika Raundi ya Pili ya mchujo kabla ya kurejeshwa kufuatia klabu ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kuondolewa kwa kumtumia mchezaji aliyekuwa amefungiwa.
    Na Sundowns hawakufanya makosa katika nafasi ya pili waliyopewa na kufanikiwa kuongoza kundi lao na kwenda kuitoa Zesco United ya Zambia kwenye Nusu Fainali kabla ya kuichapa Zamalek ya Misri katika fainali.
    Mafanikio haya yanatokana na sera nzuri za kocha Pitso Mosimane anayetaka timu ishinde kila mechi.
    Ikiwa inamilikiwa na mmoja wa matajiri makubwa wa madini Afrika Kusini, Patrice Motsepe, klabu hiyo imetamba barani kutokana na sera zake kutumia fedha kujenga timu kwa kusajili wachezaji wazuri kwa madau ya rekodi na kuwapa mishahara minono.
    Wamekwenda hadi nje ya Bara, wakimsajili beki wa kati Mbrazil, Ricardo Nascimento, aliyekuwa anacheza Ligi Kuu ya Ureno msimu uliopita na Leonardo Castro, mshambuliaji kutoka Colombia.
    Khama Billiat, mshambuliaji wao wa kimataifa wa Zimbabwe na kipa wa Uganda, Denis Onyango ni miongoni mwa wachezaji wanne wa klabu hiyo walioteuliwa kuwania tuzo ya Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika katika watano wa mwisho walioingia fainali.
    Wengine wawili ni wachezaji wa kimataifa wa Afrika Kusini, Keegan Dolly na Hlompho Kekana, ambaye ni Nahodha wa timu hiyo.
    Kocha Mosimane anatumia vizuri fursa ya utajiri wa Motsepe kuijenga klabu katika misingi ya 'kiprofesheno" kwa kuajiri makocha wasaidizi wakubwa kutoka Ulaya, madaktari na washauri- wachambuzi wa kumsaidia kuitayarisha timu vizuri.
    Sundowns inafahamika kama "The Brazilians" kwa sababu ya rangi za jezi zao kufanana na za timu ya taifa ya Brazil.
    Wataanza kampeni yao ya kuwania Kombe la Dunia Desemba 11 kwa kumenyana na mshindi kati ya Kashima Antlers ya Japan na Auckland City ya New Zealand zitakazomenyana Desemba 8. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAMELODI SUNDOWNS WAHAMISHIA UBABE WAO DUNIANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top