• HABARI MPYA

    Sunday, March 08, 2015

    OKWI ACHANA KANDAMBILI TAIFA, SIMBA SC YAIPIGA YANGA 1-0, NIYONZIMA ALIMWA NYEKUNDU

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC imeendeleza ubabe wake kwa watani, Yanga SC baada ya kuwafunga bao 1-0 jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara. 
    Sifa zimuendee mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Arnold Okwi aliyefunga bao hilo pekee kipindi cha pili.
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Martin Saanya wa Morogoro, aliyesaidiwa Soud Lila wa Dar es Salaam na Florent Zablon wa Dodoma, Yanga SC ilimaliza pungufu baada ya kiungo wake, Haruna Niyonzima kutolewa kwa kadi nyekundu, baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano.
    Emmanuel Okwi akishangilia baada ya kuifungia Simba SC bao pekee leo Taifa

    Niyonzima alionyeshwa kadi ya pili ya njano kwa ‘kujitakia’ baada ya kuupiga kutumbukiza nyavuni, wakati tayari refa Saanya amekwishapuliza filimbi ya kusimamisha mchezo.
    Okwi alifunga bao hilo dakika ya 52 kwa shuti la umbali wa zaidi ya 22 baada ya pasi ya Said Ndemla akiwa pembeni kidogo mwa Uwanja kulia, akimtungua vizuri kipa Ally Mustafa ‘Barthez’.
    Mshambuliaji Danny Mrwanda aliikosesha Yanga SC bao la wazi dakika ya 28, baada ya kupewa pasi nzuri na Simon Msuva, lakini akazubaa na mpira ndani ya boksi hadi akapokonywa na Juuko Murushid.
    Tukio hilo lilimkera kocha Mholanzi wa Yanga SC, Hans van der Pluijm ambaye alimtoa mchezaji huyo dakika mbili baadaye na nafasi yake kuchukuliwa na Hussein Javu.
    Simba SC ilitawala kwa zaidi ya asilimia 10 dhidi ya Yanga SC mchezo huo, kutokana na kulundika viungo wengi uwanjani. 
    Ushindi huo, unaifanya SImba SC ifikishe pointi 26 baada ya kucheza mechi 17 na kupanda hadi nafasi ya tatu nyuma ya Azam FC yenye pointi 30 na Yanga SC 31.
    Mshambuliaji wa Simba SC, Ibrahim Hajib kulia akijaribu kumtoka beki wa Yanga SC, Kevin Yondan kushoto
    Winga wa Yanga SC, SImon Msuva akimtoka beki wa Simba SC, Mohammed Hussein 'Tshabalala'

    Hii inamaanisha Simba SC imerejea kwenye mbio za ubingwa, kwani iwapo itaendelea kufanya vizuri na wapinzani Azam na Yanga wakateleza, mambo yanaweza kugeuka. 
    Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Ivo Mapunda, Hassan Kessy, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Hassan Isihaka, Juuko Murushid, Abdi Banda/Simon Sserunkuma dk88, Ramadhani Singano ‘Messi’, Jonas Mkude, Ibrahim Hajib/Elias Maguri dk75, Said Ndemla, Emmanuel Okwi. 
    Yanga SC; Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Said Juma ‘Kizota’, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Amisi Tambwe, Danny Mrwanda na Mrisho Ngassa/Kpah Sherman dk77.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: OKWI ACHANA KANDAMBILI TAIFA, SIMBA SC YAIPIGA YANGA 1-0, NIYONZIMA ALIMWA NYEKUNDU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top