• HABARI MPYA

  Jumapili, Machi 22, 2015

  AZAM FC YAIZIMA COASTAL UNION MKWAKWANI 1-0 MAMBO YA BOCCO

  Na Mahmoud Zubeiry, TANGA
  AZAM FC imeibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji Coastal Union, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo. 
  Shukrani kwake, mfungaji wa bao hilo Nahodha John Raphael Bocco ‘Adebayor’ dakika ya 31 akimalizia pasi nzuri ya kiungo Mudathir Yahya.
  Mpira uliozaa bao hilo ulianzia kwa winga Mganda, Brian Majwega aliyemlamba chenga beki Mbwana Hamisi ‘Kibacha’ na kutia krosi ambayo awali Bocco na Mrundi, Didier Kavumbangu walijaribu bila mafanikio kuiunganishia nyavuni.
  Ndipo mpira ukamkuta Mudathir ambaye awali alimtoka Hamad Juma na kutia krosi ya chinichini iliyozuiwa na mabeki wa Coastal na kumkuta tena kiungo huyo wa Azam FC, aliyempasia mfungaji.
  John Bocco kulia akipongezwa na Didier Kavumbangu baada ya kuifungia timu yake bao pekee dhidi ya Coastal leo
  John Bocco kushoto akijiandaa kupiga mpira dhidi ya beki wa Coastal, Hamad Juma
  Brian Majwega akimuacha chini Mbwana Hamisi 'Kibacha' kabla ya kutia krosi iliyozaa bao
  Didier Kavumbangu akimtoka beki wa Coastal, Hamad Juma

  Pamoja na kufungwa, Coastal walicheza vizuri, lakini wakashindwa kutumia vizuri nafasi kadhaa walizotengeneza, hususan kipindi cha kwanza.
  Coastal Unionleo ilianza bila ya wachezaji wake kadhaa wa kikosi cha kwanza, kama kipa Shaaban Kado na kiungo Godfrey Wambura, lakini kipa chipukizi aliyepandishwa kutoka timu ya vijana, Fikirini Bakari alifanya vizuri.
  Ushindi huo, unaifanya Azam FC ifikishe pointi 36 baada ya kucheza mechi 18, ikizidiwa pointi moja na vinara, Yanga SC.
  Kikosi cha Coastal Union kilikuwa; Fikirini Bakari, Mbwana Hamisi ‘KIbacha’, Hamad Juma, Yussuf Chuma, Tumba Swedi, Abdallah Mfuko, Joseph Mahundi/Mtenje Juma dk46, Hussein Swedi, Suleiman Rajab, Rama Salim na Itubu Imbem/Yayo Lutimba dk46.
  Azam FC; Aishi Manula, Shomary Kapombe, Erasto Nyoni, Aggrey Morris, Serge Wawa/Said Mourad dk64, Mudathir Yahya, Himid Mao, Frank Domayo/Amri Kiemba dk84, John Bocco, Didier Kavumbangu/Gaudence Mwaikimba dk72 na Brian Majwega.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AZAM FC YAIZIMA COASTAL UNION MKWAKWANI 1-0 MAMBO YA BOCCO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top