• HABARI MPYA

  Alhamisi, Machi 26, 2015

  MATUMLA: NJOONI MUONE NAVYOMUADHIBU MCHINA KESHO DIAMOND

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  BONDIA Mohamed Matumla amewaahidi furaha Watanzania kesho atakapopambana na Mchina, Wang Xin Hua katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.
  Akizungumza wakati wa kupima uzito leo, Dar es Salaam Matumla amesema kwamba amejindaa vizuri kwa ajilo ya kushinda mchezo huo wa uzito Super Bantam.
  Pambano hilo ni la kuwania nafasi ya kugombea taji la dunia la WBF, Mei 2, mwaka huu mjini Las Vegas, Marekani siku ambayo Manny Pacquiao wa Ufilipino atapigana na Mmarekani Floyd Mayweather Jr.
  Yaani mshindi wa pambano kati ya Matumla Jr na Xin Hua atapata tiketi ya kwenda kupigana katika pambano la utangulizi la Mayweather na Pacquiao Mei 2, Marekani. 
  Mohamed Matumla kulia na mpinzani wake, Wang Xin Hua kushoto. katikati ni promota Jay Msangi, aliyeandaa pambano hilo
  Mohammed Matumla kulia akitunishiana misuli na mpinzani wake, leo wakati wa kupima uzito

  “Namshukuru Mungu nimejiandaa vizuri, na niko vizuri kabisa kuelekea pambano hilo. Nawaahidi furaha Watanzania, waje kwa wingi kunishangilia ili kunihamasisha,”amesema mtoto huyo wa bingwa wa zamani wa dunia, Rashid Matumla.
  Kwa Mohamed ‘Mudy’ hilo litakuwa pambano ake la 17 tangu aanze ngumi za kulipwa miaka mitatu iliyopita akiwa ameshinda mara 11, manne kwa Knockout (KO), amepoteza mawili, yote kwa pointi na sare nne.
  Pambano hilo litatanguliwa na mapambano kadhaa mengine, yenye mvuto, likiwemo kati ya Ashraf Suleiman wa Tanzania dhidi ya Mmarekani, Joseph Rabotte uzito wa juu taji la International WBF.
  Mabondia wa Tanzania, Karama Nyilawila na Thomas Mashali watachapana katika pambano la uzito wa Super Middle kuwania taji la WBF Intercontinental, wakati Japhet Kaseba na Maada Maudo watachapana katika uzito wa Light Heavy kuwania ubingwa wa Taifa.    
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MATUMLA: NJOONI MUONE NAVYOMUADHIBU MCHINA KESHO DIAMOND Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top