• HABARI MPYA

  Jumapili, Machi 29, 2015

  MATUMLA JR AMPOTEZEE MIYEYUSHO KWA SASA, AWAZE FEDHA NA MATAJI

  KAMA ni kweli, hatujaongopewa, kijana wa Tanzania, Mohammed Rashid Matumla Jr atapigania taji la dunia la WBF, Mei 2, mwaka huu ukumbi wa MGM Grand mjini Las Vegas, Marekani siku ambayo Manny Pacquiao wa Ufilipino atapigana na Mmarekani Floyd Mayweather Jr.
  Matumla Jr amefanikiwa kupata nafasi hiyo baada ya kumshinda kwa pointi Mchina, Wang Xin Hua katika pambano la mchujo kuwania nafasi hiyo, uzito wa Super Bantam usiku wa Ijumaa kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.
  Ulikuwa ni ushindi ambao haukuwa na ubishi, kwani mtoto wa bingwa wa zamani wa dunia WBU uzito wa Light Middle, alimzidi mpinzani wake mwanzo hadi mwisho katika pambano la raundi 10.

  Na haikuwa ajabu majaji wote watatu, Robert Kasiga, Sakwe Mtulya na Francois Botha walipompa ushindi Mudi Matumla.
  Kama promota Jay Msangi aliyeandaa pambano hilo alikuwa mkweli, sasa tutarajie kumuona kijana wa Tanzania akipigana katika moja ya mapambano ya utangulizi Mei 2, mwaka huu mjini Las Vegas, Marekani kabla ya Pacquiao kupigana na Mayweather Jr.
  Matumla Jr ni bondia chipukizi anayeinukia vizuri, ambaye juzi alipigana pambano la 18, akishinda kwa mara ya 12 tangu aanze ngumi za kulipwa Novemba 17, mwaka 2010.
  Katika mapambano hayo, Matumla ametoa sare mara nne na kupoteza mawili, dhidi ya Francis Miyeyusho Mei 10, mwaka jana na Emilio Norfat Januari 31, mwaka huu, yote kwa pointi tena akipigana vizuri tu.
  Ni watoto ambao, pamoja na mdogo wake, Daudi waliingia kwenye ngumi kuendeleza asili ya ukoo wao, kwani babu yao ndiye aliyefungua njia na baba zao na shangazi yao wakafuatia na sasa wao. 
  Bahati mbaya, Daudi ambaye wataalamu wanasema ndiye fundi zaidi, hajibidiishi sana na mchezo- yeye hupata hamasa anapomuona kaka yake akifanya vizuri ulingoni na kuahidi ataanza mazoezi, lakini baadaye anarudi katika maisha yake aliyoyazoea pale Keko.
  Ukweli ni kwamba juzi watu wameshuhudia ngumi nzuri baada ya muda mrefu katika ukumbi wa Diamond Jubilee. Juzi tuliona ngumi zote, jabs (za kudonoa), upper-cut (mkono kutokea chini katikati) na hooks (mkono kutokea pembeni).
  Juzi tuliona kijana anayepigana kwa staili ya baba, Rashid Matumla enzi zake akiwakalisha wapinzani na kutwaa mataji lukuki, Orthodox yaani kutanguliza mkono na mguu wa kushoto mbele. 
  Bondia wa China alionekana kuzidiwa na makonde mfululizo ya Matumla tangu raundi kwanza na akaanza kumpunguza kasi mpinzani wake kwa kusingizia anapigwa chini ya mkanda.
  Awali, alifanikiwa kumrubuni refa Mtanzania, Emmanuel Mlundwa ambaye alimkata pointi Matumla, lakini janja yake ikashitukiwa kuanzia raundi ya tano na ndipo alipoanza ‘kupigwa kama begi’. 
  Ikumbukwe kwa Tanzania, hususan Dar es Salaam bado kuna upinzani wa ngumi wa kikanda, yaani mabondia wa Kinondoni na Temeke na kwa mapromota ushindani huo umekuwa ukiwanufaisha sana kibiashara.
  Lakini pia kwa mabondia wenyewe, kutokana na siku hizi kutokuwa na mameneja wa kuwaongoza- wanashindwa kupuuzia kelele za wapinzani na kufikiria kupigana mapambano yenye manufaa zaidi na wao.
  Matokeo yake, bondia wa Keko anaweza kupigana hata mara sita na bondia wa Manzese, kisa upinzani tu ambao mwisho wa siku unawarudisha nyuma mabondia wenyewe.
  Nimesema Matumla alishindwa na Francis Miyeyusho Mei mwaka jana pale PTA. Miyeyusho ni bondia ambaye hapo kabla, alimpiga baba yake mdogo Mohammed, Mbwana Matumla.
  Chichi Mawe ‘alichonga’ sana baada ya ushindi wake wa pointi PTA- akimtambia Mudi Matumla eti hata aende na ukoo wake wote, bado atawapiga tu.
  Nilizisoma hisia za Mudi, alikuwa ana hasira za Miyeyusho na kama amemuwekea nadhiri lazima siku moja amtandike ulingoni. Mimi ni mmoja wa watu wanaoamini Mudi Matumla atakuja kumpiga vibaya sana Francis Miyeyusho siku moja.
  Kwa nini naamini hivyo? Francis anaelekea ukingoni kimchezo na Mudi ndio anachipukia na hata Mei mwaka jana ilikuwa mapema sana kuwakutanisha wawili hao.
  Lakini kwa nini Mudi afikirie kulipa visasi, badala ya kufikiria kutafuta fedha zaidi kupitia mchezo ambao Mungu amemjaalia kipaji.
  Baba yake ana nyumba zisizopungua tano Dar es Salaam ambazo zote alijenga kutokana na fedha alizokuwa analipwa enzi zake anapigana.
  Sasa Rashid Matumla ameweka wapanganji katika nyumba zake, anakusanya fedha za kodi zinamsaidia kuendesha maisha yake- huku pia akipiga deiwaka za kuwafundisha mabondia- wakati huo huo akiwa kocha wa watoto wake mwenyewe.
  Mudi akitekwa na mawazo ya kishabiki na kufikiria kurudiana na Miyeyusho hivi karibuni, badala ya kufikiria kupata aina ya mapambano yatakayomjenga zaidi na kuzidi kumfungulia njia ya mafanikio, atajimaliza.
  Nimesema naamini siku moja Mudi Matumla atampiga Francis Miyeyusho, lakini si hivi karibuni- angalau baada ya mwaka zaidi.
  Narudia, kama ni kweli Mudi atakuwa na pambano Mei Marekani, basi kwa sasa aelekeze nguvu zake kwenye maandalizi ya pambano lake lijalo, baada ya mapumziko mafupi.
  Na baada ya pambano hilo pia, Mudi anapaswa kutengenezewa mipango ya kupata wapinzani wa nje, kutengeneza rekodi na kuwania mataji- ili pia kama baba zake, Rashid na Mbwana, naye ailetee sifa nchi.
  Huo ndiyo ukweli, si huwa tunasema Tanzania imekwishatoa mabingwa wa dunia na wa kwanza alikuwa Rashid Matumla- basi kila la heri kwa Matumla Jr, ila kwa sasa aache kumfikria Miyeyusho, aelekeze fikira zake mbele akavune fedha na mataji. Jumapili njema.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MATUMLA JR AMPOTEZEE MIYEYUSHO KWA SASA, AWAZE FEDHA NA MATAJI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top