• HABARI MPYA

  Jumamosi, Machi 28, 2015

  MATUMLA JR AMUADHIBU MCHINA, SASA KUPANDA ULINGO MMOJA NA MAYWEATHER, PACQUIAO MEI 2 LAS VEGAS

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MTANZANIA Mohammed Rashid Matumla amewafurahisha Watanzania kama alivyoahidi baada ya kumshinda kwa pointi Mchina, Wang Xin Hua katika pambano la uzito wa Super Bantam usiku huu ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.
  Ulikuwa ni ushindi ambao haukuwa na ubishi, kwani mtoto wa bingwa wa zamani wa dunia WBU uzito wa Super Middle, alimzidi mpinzani wake mwanzo hadi mwisho katika pambano la raundi 10.
  Na haikuwa ajabu majaji wote watatu, Robert Kasiga, Sakwe Mtulya na Francois Botha walipomshinda Matumla Jr- na sasa kijana huyo atapigana taji la dunia la WBF, Mei 2, mwaka huu mjini Las Vegas, Marekani siku ambayo Manny Pacquiao wa Ufilipino atapigana na Mmarekani Floyd Mayweather Jr.
  Mohammed Matumla kulia akimuadhibu mpinzani wake, Wang Xin Hua usiku huu
  Mohammed Matumla alitawala pambano mwanzo hadi mwisho
  Refa Emmanuel Mlundwa akimuinua mkono Mohammed Matumla kumtangaza mshindi dhidi ya Wang Xin Hua

  “Lilikuwa pambano gumu, lakini ninamshukuru Mungu nimeshinda na kuwafurahisha Watanzania ambao walijitokeza kwa wingi kunisapoti. Ushindi huu ni matokeo ya maandalizi mazuri chini ya kocha wangu, baba yangu (Rashid Matumla),” alisema Matumla Jr, ambaye hilo linakuwa pambano lake la 12 kushinda kati ya 18, aliyocheza tangu aanze ngumi za kulipwa miaka mitatu iliyopita, akiwa amepoteza mawili, yote kwa pointi na sare nne.
  Bondia wa China alionekana kuzidiwa na makonde mfululizo ya Matumla tangu raundi kwanza na akaanza kumpunguza kasi mpinzani wake kwa kusingizia anapigwa chini ya mkanda.
  Awali, alifanikiwa kumrubuni refa Mtanzania, Emmanuel Mlundwa ambaye alimkata pointi Matumla, lakini janja yake ikashitukiwa kaunzia raundi ya tano na ndipo alipoanza ‘kupigwa kama begi’ 
  Katika mapambano ya utangulizi, bondia wa kike, Bena Kariuki alimshinda Mtanzania, Asha Ngedere kwa Knockout (KO) raundi ya nne, uzito wa Light Welter na kutwaa taji la UBO International, wakati Ashraf Suleiman alimshinda kwa Technical Knockout (TKO) raundi ya nne uzito wa Heavy.
  Karama Nyilawila alimshinda TKO raundi ya nane Ibrahim Tamba uzito wa Super Middle kuwania taji la WBF Intercontinental, Mada Maugo alimshinda Japhet Kaseba kwa TKO raundi ya nane uzito wa Light Heavy kuwania ubingwa wa Taifa. 
  Cossmas Cheka aimshinda kwa pointi Mfaume Mfaume pambano la uzito wa Light Walter na Koba Donati alimshinda kwa pointi Baina Mazola pambano la uzito wa Feather.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MATUMLA JR AMUADHIBU MCHINA, SASA KUPANDA ULINGO MMOJA NA MAYWEATHER, PACQUIAO MEI 2 LAS VEGAS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top