• HABARI MPYA

    Sunday, March 22, 2015

    MIAKA 20 BILA `JABALI LA MUZIKI` MARIJAN RAJABU, PENGO LAKE HALIJAZIBIKA

    Na Hemed Kivuyo, DAR ES SALAAM
    Kwa Bahati Nzuri Nilianza shule ya Msingi nikiwa nafahamu kusoma na kuandika, Nilikuwa Nasoma Magazeti yaliyokuwa yakiletwa na Baba Yangu (Issihaka Kivuyo) mengine nilikuwa nakwenda nayo shule nakusoma hukohuko.
    Nilipokuwa narejea Nyumbani  Nilikuwa namkuta Mama Yangu ( Amina Salim Arajiga) akiskiliza Radio ( Radio Tanzania) mara nyingi muda niliyotoka shule kulikuwa na Kipindi cha `Chaguo la msikilizaji`.
    Nilikuwa namkuta Mama akiimba nyimbo za Marijani zilizopigwa Radioni nayeye huiga kwakuzifuatisha. Nyimbo kama `mama fatu, Hellena, Namsaka Mbaya Wangu, Georgina, Masoud. Kabla sijajua nani aliziimba nilimsikia akiziimba Mama Yangu.
    Marijan Rajab enzi za uhai wake akiimba

    Mama alikuwa akiimba huku akitikisa kichwa huku akisema `jamani Marijani anaimba!!! Alimsifu sana Marijan  kwa Tungo zake zilizojaa mafundisho. Mama Yangu aliniambukiza nami nikajikuta napenda nyimbo za Marijan na kufuatilia na hata historia yake.
    Machi 23 mwaka 1995 Nikiwa shule ya Msingi, Marijan Rajab aliaga Dunia na kuzikwa kesho yake machi 24  katika makaburi ya Kisutu Jijini Dar es salaam. Hapana Shaka ni miaka 20 sasa tangu Jabali la Muziki, Nguli, Marijan Rajab aage Dunia. Jabali aliaga Dunia akiwa na umri wa miaka 40.
    Mbali na Muziki Marijani alikuwa si tu mpenda Soka bali pia alikuwa Golikipa wa timu ya Soka ya Simba na hata shuleni alikuwa Golikipa wa timu ya Shule yake.
    Kama umefuatilia historia ya Marijan vyema hutohitaji kuwa na Elimu ya juu kutambua `kipaji` cha Marijan ambacho sijaona mfano wake mpaka sasa. Ni Mwendawazimu pekee atakayekosa macho ya kuona `upekee wa Marijan`.
    Marijani Rajab alitunga tungo zinazoendelea kuishi mpaka sasa na hapana shaka yeyote ataendelea kuishi katika Dunia ya Muziki dahari na dahari.
    Katika Tungu Marijan aliweza kuishi katika jambo analoimba, akiimba ukewenza basi anauvaa uhusika. Ukitaka kuamini hilo hebu sikiliza wimbo unaoitwa `mama fatu au ukewenza. Si tu sauti muruwa ni mashairi yanayoishi na yataendelea kuishi kutokana na aliyoimba kuendelea kutokea kila uchwao.
    Katika Wimbo wa Mapenzi Marijani alivaa uhusika hasa. Hebu Sikiliza wimbo `Aisha ,au mtoto wa Mwanza. Katika kufundisha wanandoa hebu sikiliza wimbo uitwao Siwema namba mbili. Umsikie binti aliyeolewa na Sadiki lakini rafiki zake wakampotosha na kumwambia `sadiki atakupa nini siwema? Twende zetu tukapate raha za dunia, kwanza atakuweka ndani kama pazia,hebu jitizame ulivyoumbika. ( kabla sijaendelea niseme wazi tu kwamba wimbo huu hunitoa matozi kila niusikiapo,huwa najuta kuusikia)
    Marijani aliimba Nyimbo za Kikombozi,ukombozi wa Afrika kupinga unyonyaji na kila aina ya ukatili,Sikiliza wimbo wake uitwao `Sikitiko`. ( Marijani hebu amka uone uliyomba yakiendelea kushamiri kaka yangu``)   Heshima ya Mtu nikazi,zuwena. Na Ndiyo maana nasema hakuna kama Marijani Rajab na hatotokea tena.
    Nasema hatotokea Tena kwasababu huu `uwendawazimu` unaoitwa kwenda na wakati ndiyo unazidi kushika kasi.
    Alipokaribia takriban miaka 18, nyota yake katika muziki ilianza kung’aa, baada ya kujiunga na bendi ya STC Jazz .
    Bendi hiyo ilikuwa chini ya mpiga gitaa maarufu wakati huo, Raphael Sabuni. Kabla ya hapo, bendi hiyo ilikuwa inajulikana kama The Jets.
    Akiwa na bendi hiyo, aliweza kusafiri nje ya Tanzania kwa mara ya kwanza, ambapo alikwenda  nchini Kenya. Aliambatana na bendi yake kwa madhumuni ya kwenda kurekodi nyimbo, ambazo zilitoka katika chapa ‘label’ ya Phillips.
    Mwaka 1972, Marijani alihamia bendi ya Safari Trippers. Hapo ndipo ubora wake ulifunguka hasa, kwa kuweza kuinyanyua Trippers, kuwa miongoni mwa bendi maarufu hapa nchini wakati huo.
    Waliweza kutoa vibao vilivyopendwa mfululizo, pia walifanya ziara ya kuzunguka nchi nzima.
    Vibao kama ‘Rosa Nenda Shule’, ‘Georgina’ na ‘Mkuki Moyoni’ viliweza kuuza zaidi ya nakala 10,000 za santuri, hivyo kuwezesha bendi kununua vyombo vyake vizuri.
    ‘La kuvunda halina ubani’, msemo huu ulijionesha wazi pale maelewano mabaya kati ya wanahisa wanne wa Safari Trippers yaliposababisha kusambaratika kwa bendi hiyo, licha ya kuwa juu kimuziki wakati huo.
    Miezi michache baadaye, Marijani na wenzake waliibukia katika bendi ya Dar International. Huko waliwakuta wanamuziki wengine wazuri. Kwa mshikamano wa pamoja, wakaongeza nguvu na kuifanya bendi hiyo kupata umaarufu wa hali ya juu. Vibao vya ‘Zuwena’ na ‘Mwanameka’ vilitamba katika vipindi kadhaa vya salamu vya Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD), wakati huo.
    Kwa wakati ule, bendi yao ilirekodi vibao hivyo katika studio hizo za RTD, iliambulia kupata sh 2,500 tu.
    Kati ya mwaka 1979 na 1986, Dar International ilipita kila wilaya hapa nchini kupiga muziki, kwa ajili ya kutoa elimu sambamba na kuwaburudisha wananchi, wakipiga katika mtindo wao wa ‘Super Bomboka’.
    Uchakavu wa vyombo hatimaye mwaka huo wa 1986 ukamaliza mbio za bendi hiyo.
    Historia inaeleza kuwa Marijani Rajabu ‘Jabali la Muziki’ alikuwa mmoja wa wanamuziki 57 waliounda kundi la wasanii likijulikana kama Tanzania All Stars mwaka 1987.
    Kundi hilo lilitia fora kwa wimbo wake wa ‘Fagio la Chuma’Kundi hilo lilirekodi vibao vingine vinne, ambavyo si rahisi kwa bendi zilizopo sasa kufikia ubora wake kimuziki.
    Marijani Rajabu alipiga hodi katika Jiji la Arusha na akajiunga na bendi ya Kurugenzi Jazz, ambako alidumu kwa mwaka mmoja.
    Baada ya kuhangaika huku na kule, baadaye Marijani Rajabu akaamua kuthubutu kuanzisha kundi lake likiitwa Africulture.
    Kundi hilo lililotamba katika mtindo wake wa ‘Mahepe’, halikudumu muda mrefu kutokana na ukosefu wa vyombo vya muziki. Hatimaye mambo yakawaendea kombo, tofauti na walivyotarajia.
    Maisha ya mwanadamu yana majaribu mengi sana. Inaelezwa kwamba, kufikia mwaka 1992, hali ya maisha ya Marijani ilikuwa ngumu mno. Alifikia kuendesha maisha yake kwa kuuza kanda za nyimbo zake.
    Pamoja na nyimbo nyingi za kuimbia chama tawala na serikali, hata tungo yake ‘Mwanameka’ kutumiwa katika mtihani wa kidato cha nne.
    Marijani Rajabu hakuwahi kukumbukwa rasmi kama mmoja wa wasanii bora Afrika Mashariki, hadi mwishoni mwa mwaka jana, alipotunukiwa nishani ya heshima ya Muungano na Rais Jakaya Kikwete, siku ya maadhimisho ya miaka 51 ya Uhuru wa Tanzania Bara, zilizofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru Desemba 9, 2012 jijini Dar es Salaam.
    Aliacha Tungo Nyingi sana  ‘Masudi’, ‘Habari yako’, ‘Sauti Yako Nyororo’, ‘Baba Anna’, ‘Kitinda Mimba’ na ‘Salama Nakuita’. Marijani alifyatua vingine vya ‘Tabu Ni Hali ya Dunia’, ‘Ndoa ya Mateso’, ‘Namsaka Mbaya Wangu’, ‘Tamaa Mbele’ na ‘Baba Watoto’.
    INNAH LAAH WAINNAH LILAHY RAJUUN. MLAZE PEMA MARIJANI RAJABU
    (Mwandishi wa makala haya ni mtangazaji wa Redio One na ITV na anapatikana kwa namba +255 752 250 157 na +255 655 250 157)
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MIAKA 20 BILA `JABALI LA MUZIKI` MARIJAN RAJABU, PENGO LAKE HALIJAZIBIKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top