• HABARI MPYA

    Wednesday, March 25, 2015

    USHINDI NI WA WALOZI, MAKOCHA NA WACHEZAJI NI KWA AJILI YA KUFUNGWA!

    INAAMINIKA uchawi ni imani za Kiafrika na Waafrika, ingawa ukweli ni kwamba hata nchi nyingine za Asia, Amerika na Ulaya zinaabudu uchawi.
    Kwa waumini wa dini ya Kiislamu, ambayo mimi ni miongoni mwao, uchawi ni katazo, ambalo limetiliwa msisitizo mkuu, kwamba anayefanya hivyo, basi hamuamini Mungu.
    Au, anamshirikisha Mungu wake katika uovu na hiyo ni dhambi kubwa. Vivyo hivyo, hata kwa waumini wa dini nyingine, uchawi unakatazwa.
    Lakini bado unaweza kuona pamoja na imani na makatazo yote, uchawi una historia ndefu na simulizi za vitabu tunavyoviamini kiimani zinatueleza hata Mitume wa Mungu walijaribiwa.

    Pamoja na yote, bado watu wanaomuamini Mungu kwa dhati hawayumbishwi wala kutikiswa na uchawi kwa namna yoyote.
    Tunaamini, uchawi unatumika na wengi katika harakati za maisha, lakini kwa kiasi kikubwa umekuwa ukitumiwa na wanamichezo na wasanii.
    Wapo wanaotumia uchawi eti kusafisha nyota zao, na wengine eti kuwaloga wenzao wasifanye vizuri zaidi yao na bahati mbaya imani hiyo imezidi kuenea za kuzidi kupotosha vizazi na vizazi.
    Wenye kupata mafunzo ya kidini wangali wadogo wanakuwa na imani kwamba uchawi ni uongo, utapeli na dhambi kubwa- hao hata katika maisha yao ya kawaida huwa ni hivyo.
    Waliochimba zaidi wanaweza wakawa wanakubali uchawi upo, lakini wakaamini ni wa shetani na wakasimama imara kupambana nao.
    Binafsi naweza kuwa nina bahati, kutoka kwenye familia, shule nilizopitia, walimu walionisomesha walikuwa hawaaamini, au hawaukubali uchawi.
    Na hayo yakawa mafundisho niliyoshika mapema, ingawa katika pilika nyingine za maisha nilikutana na hila za kichawi na ushirikina.
    Nasema hila kwa sababu siamini na ninamuomba Mungu ninayemuamini azidi kuishika nafasi yangu, isije kuingia majaribuni katika hilo.
    Kwa nini leo nimekuja na hadithi za uchawi na ushirikina? Nitawaambia.
    Wakati tukiwa wadogo, tulisimuliwa hadithi nyingi za kifimbo cha marahemu baba wa taifa letu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwmaba eti kilikuwa cha miujiza inayohusishwa na uchawi.
    Lakini katika utu uzima wangu nilipoanza kusikiliza hotuba za marehemu Mwalimu, zinaonyesha hakuwa mshirikina hata kidogo. Ila nimekuwa nikijiuliza, kati ya waliosimuliwa kuhusu kifimbo cha Mwalimu, ni wangapi walibahatika kujiridhisha ilikuwa ni uzushi.
    Wakati fulani niliwahi kuchezea timu ya Nungu ya Kariakoo, tulikuwa na kocha wetu mmoja alikuwa anaitwa Msimu Said Msemwa, alikuwa anapenda kusema; “Uzushi unaenea kama ushuzi”- akimaanisha mtu anajamba mwenyewe kimya kimya, lakini harufu ya ushuzi inaenea haraka na watu wanaanza kusikia kichechefu. 
    Vivyo na habari za ‘kuupromoti’ ushirikina kwa kutumia majina ya watu wakubwa na maarufu ni uzushi unaoenezwa na kuenea haraka kama ushuzi.
    Leo wapo wapenzi wa michezo wanasimuliana eti Didier Drogba alimloga Fernando Torres baada ya kusajiliwa Chelsea kwa dau la rekodi, Pauni Milioni 50 kutoka Liverpool.
    Labda Drogba anapakaziwa hivyo kwa sababu ni Mwafrika mwenzetu, lakini tujiulize kipi kimemzima ghafla Robin van Persie pale Manchester United?
    Mafanikio ya wachezaji wengine bora kuwahi kutokea Afrika kama Rogger Milla na Samuel Eto’o pia yamekuwa yakihusishwa na imani za kishirikina, lakini najiuliza tu, kwa nini magwiji hawa hawakuongeza hilo juju wawe Wanasoka Bora wa Dunia?
    Asamoah Gyan anazushiwa hadi kumuua rafiki yake kipenzi,  Theophilus Tagoe ‘Castro’ aliyekuwa mwanamuziki ili kumtoa kafara.
    Huo ni uzushi ambao Gyan mweyewe alishindwa kuuvumilia, akaibuka kukanusha akisema tetesi hizo ni za kushangaza sana na wala hazina msingi.
    Lakini Gyan huyu ni ambaye kwa sasa anaelekea kutungika daluga zake, akiwa hajafikia mafanikio ya maana sana katika soka- je, kwa nini asiloge ili angalau awapiku akina Yaya Toure, Eto’o na Drogba?
    Nchini Tanzania hatuko nyuma kwa imani za kishirikina kwenye michezo.
    Wakati fulani mabondia Rashid Matumla na mdogo wake, Mbwana walikuwa wanafanya vizuri kwenye ndondi na mafanikio yao yakahusishwa na uchawi.
    Lakini Mungu akawadhihirishia wanadamu wa Tanzania kwamba, vijana hao walifanya vizuri kwa uwezo na vipaji vyao, kwani umri ulipowatupa mkono na uwezo kupungua, waligeuka kuwa wa kupigwa pigwa.
    Siku moja, tulikuwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro na Edo Kumwembe tunashuhudia Francis Cheka akimuadhibu Rashid Matumla kama mtoto mdogo.
    Kwa Edo, nadhani lile lilikuwa miongoni mwa mapambano ya mwanzoni sana ya ngumi kuangalia, alimuhurumia sana Rashid. Lakini mimi nilijiridhisha kwa mara nyingine, akina Matumla walitamba kwenye ndondi kwa uwezo na vipaji vyao, ambavyo vilipoisha wakaanza kuchezea vichapo.
    Ni kama Mike Tyson tu wakati wake, alikuwa anawatandika watu ‘kinyama’, lakini naye uwezo ulipoisha, alichapwa sana tu.
    Yote haya yanaweza yakawa sababu za kutufanya tuukatae ushirikina kwenye michezo. 
    Moja ya maeneo kwenye michezo Tanzania ambayo ushirikiana unaabudiwa sana ni kule kunakoitwa Simba na Yanga.
    Ushirikina Simba na Yanga, si kwa wachezaji na makocha pekee, bali hata viongozi wanatajwa.
    Muongo mmoja uliopita kiongozi mmoja mwenye asili ya Kiasia wa Simba SC, alihusishwa sana na vifo vya viongozi wenzake ambao alikuwa anapingana nao.
    Mwenyekiti wa Yanga SC, Yussuf Manji aliwahi kutoa Sh. Milioni 40 kuwapa wazee wa klabu hiyo wakaloge, lakini timu ikafungwa 1-0 na Simba Morogoro  Oktoba 24, mwaka 2007.
    Lakini ajabu baada ya kipigo hicho cha bao la Ulimboka Mwakingwe Uwanja wa Jamhuri, kipa wa Yanga SC, Ivo Mapunda akasimamishwa eti alihujumu timu. Na wale wazee zile Milioni 40 walipeleka wapi? Kama waliwapa wachawi kwa nini timu ilifungwa?
    Na imekuwa ndiyo desturi, kila mechi ya Simba na Yanga bajeti za ‘wataalamu’ zinatengwa na timu ikishinda, inadaiwa huwa wanaongezewa fedha. 
    Ajabu tu ni kwamba, timu inapofungwa, watu wanasahau kwamba kuna fedha zilipelekwa kwa walozi, wanaanza kutupia lawama wachezaji na makocha.
    Tumeshuudia sana wachezaji na makocha wakifukuzwa Simba na Yanga kwa ajili ya timu kufungwa, lakini hao wachawi huwa wanachukuliwa hatua gani? 
    Tuache kudanganyana, uchawi mzuri ni kusajili wachezaji bora na kuandaa timu vizuri.   Huo ndiyo uchawi ambao hata Sumbawanga wakianza kuutumia leo, watakuwa na timu Ligi Kuu. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: USHINDI NI WA WALOZI, MAKOCHA NA WACHEZAJI NI KWA AJILI YA KUFUNGWA! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top