• HABARI MPYA

  Jumatatu, Machi 23, 2015

  MSIMU WA KILIMANJARO TANZANIA MUSIC AWARDS 2015 WAZINDULIWA RASMI LEO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  BARAZA la Sanaa Tanzania (BASATA) kwa kushirikiana na Kilimanjaro Premium Lager leo wamezindua rasmi msimu mwingine wa tuzo za muziki Tanzania unaojulikana kama Kilimanjaro Tanzania Music Awards (KTMA). Uzinduzi huu ulifanyika kwenye ukumbi mpya wa LAPF uliopo barabara ya Ali Hassan Mwinyi jijini Dar es Salaam.
  Akizungumza na Waandishi wa Habari mjini Dar es Salaam leo, Meneja wa bia ya Kilimanjaro Pamela Kikuli amesema muda wa kuwatunza wasanii wa muziki waliofanya kazi nzuri zilizokubalika na wengi umewadia. “Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, ni bia ya watanzania, na imejikita katika kuwaletea burudani na pia kutoa majukwaa ambayo yanawapa Watanzania fursa ya kukuza vipaji mbalimbali, likiwemo jukwaa la muziki la Kilimanjaro Tanzania Music Awards.” Aliendelea “Na hii tumeithibitisha kwa juhudi za makusudi za kutenga fungu kubwa na kuongeza ushiriki wa wataalaam mbali mbali kwenye fani husika ili kuziendeleza, kuzikuza na kuziongezea thamani tuzo hizi mwaka hadi mwaka sambamba na umaarufu kuongezeka kwenye medani za Kimataifa.”
  Diamond Platinumz kulia aling'ara katika tuzo za Kili mwaka jana

  Kilimanjaro Premium Larger inawekeza zaidi ya billion moja shilingi za ki Tanzania kuhakikisha ubora wa hali ya juu unajitokeza kwenye mchakato mzima wa tuzo hizi. “Bia ya Kilimanjaro itaendelea kuwekeza kwenye mambo yetu na kuyasimamia kikwetu kwetu!” Pamela Kikuli.
  Msimu huu hauna mabadiliko makubwa sana katika vipengele wala mfumo wa kuwapata wateule, bali kuna maboresha kwenye njia za upigaji kura ili kuongeza ufanisi na pia kuendeleza utaratibu wa kufanya mambo yetu ya KTMA ki kwetu kwetu. Kwa mfano Tanzania sasa inawatu zaidi ya milioni mbili na laki tano kwenye whatsapp, KTMA imewarahisishia kwa kuongeza njia hiyo kwenye mchakato wa kupendekeza na kupiga kura.
  Mchakato wa kuwapata wateule utapitia ngazi mbali mbali hadi kuwapata washindi na kutangazwa kwenye usiku wa utoaji tuzo. 

  Ratiba ya KTMA 2015:
    Tukio Mwezi Tarehe
  1 Uzinduzi Machi 23
  2 Mchakato wa Mapendekezo Machi/Aprili 30/19
  3 Academy Aprili 25
  4 Kutangaza wateule Aprili 27
  5 Semina ya Wateule Aprili 30
  6 Kura za ushindi Mei 1-31
  7 Gala Night Juni 13

  Upande mwingine BASATA ilitangaza kuanza kwa kura za mapendekezo kutoka kwa wapenzi wa muziki nchini. “Kama tulivofanya mwaka jana na mwaka huu Tanzania itatoa maoni ya nani aingie kwenye kinyang’anyiro.” Alisema Katibu Mtendaji wa BASATA Nd. Godfrey Mngereza. 
  Kura za maoni zitaanza tarehe 30/Machi hadi 19/Machi 2015. Shabiki ataweza kupendekeza nani ama nyimbo zipi ziwemo kwenye vipengele vyote vya KTMA 2015. Kwa mfano: Wimbo bora wa mwaka, shabiki wa muziki ana nafasi ya kupendekeza nyimbo zote tano ambazo anaona ni bora na zina kidhi vigezo vya BASATA kwa mwaka 2015. “Ni muhimu kuelewa kwamba mapendekezo yote ni lazima yatokane na vigezo vya BASATA. Kama wimbo haukupata umaarufu, haukushika chati, haukupigwa kwenye vyombo mbali mbali vya burudani (yaani media channels), hauwezi kuwa na vigezo vya kupendekezwa’ alisema Bw. Mngereza.
  Kura mwaka huu kwenye ngazi zote zitapigwa kwa njia kuu tatu; mtandao, Whatsapp na SMS. Njia zote hizi zitahitaji namba hai ya simu ili kukamilisha zoezi. Kipindi cha kupiga kura za kuchagua washindi utaratibu wa namba moja ya simu kupiga kura moja utaendelea. Haijalishi njia ipi mpiga kura atatumia lakini namba moja kura moja kwa kipengele kimoja. “Ukipigia kura kipengele kwa njia ya whatsapp, hautaweza kuipigia kura tena kipengele hicho kwa kutumia SMS au kwenye mtandao”. Alifafanua Pavel Gabriel wa Auditax International.

  Njia za kupiga kura ni kama zifwatazo:
  1. Whatsapp – 0686 528 813.
  2. SMS – 15415.
  3. Mtandao – www.ktma.co.tz 

  BASATA wameendelea kusisitiza usimamizi wa maingizo ya nyimbo kuendelea kufanywa kwa umakini mkubwa na kwa kushirikiana kwa karibu zaidi na AUDITAX INTERNATIONAL – kampuni inayosimamia mchakato mzima. Katibu Mkuu wa BASATA alisisitiza kwamba ‘Kama kuna wimbo ulifungiwa na BASATA hautaruhusiwa kushiriki kwenye mchakato’ BASATA.
  Katibu Mkuu wa BASATA amehimiza mashabiki wa muziki watumie fursa kuwapendekeza wasanii wanaowashabikia kazi zao kwenye vipengele husika kuanzia tarehe 30.03.2015. BASATA wameshauri kuzingatia vigezo vya kila kipengele ambavo vitachapishwa kwenye magazeti na kuwekwa kwenye mitandao mbali mbali.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MSIMU WA KILIMANJARO TANZANIA MUSIC AWARDS 2015 WAZINDULIWA RASMI LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top