• HABARI MPYA

    Friday, March 27, 2015

    JUUKO WA SIMBA AMSONONESHA MICHO, ASIKITISHWA PIA NA WINGA WA AZAM, MAJWEGA KUIPUUZA TIMU YA TAIFA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KOCHA wa timu ya taifa ya Uganda, Mserbia Milutin Sredojevic ‘Micho’ amesikitika kuwakosa wachezaji wake wawili wanaocheza Tanzania, beki Juuko Murushid na winga Brian Majwega katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa juzi dhidi ya Nigeria.
    Uganda iliifunga 1-0 Super Eagles Uwanja wa Akwo Ibom mjini Uyo, juzi usiku bao pekee la Farouk Miya dakika ya 81, akimtungua kipa bora Afrika Vincent Enyeama ambaye alikuwa anacheza mechi yake ya 100 Eagles.
    Enyeama anakuwa mchezaji wa pili wa Nigeria, baada ya beki Joseph Yobo kufikisha mechi 100.
    Micho aliwaita kikosini kwa ajili ya mechi hiyo, beki wa Simba SC, Juuko Murushid na winga wa Azam FC, Brian Majwega.
    Juuko Murushid aliruhusiwa na Simba SC kwenda kuichezea Uganda, lakini 'akabana' uswahilini Dar es Salaam

    Hata hivyo, wachezaji hao licha ya kutumiwa tiketi hawakwenda Nigeria na Micho hajafurahishwa na hilo, ingawa amesema; “Nashukuru tumeshinda bila wao,”.
    Rais wa Simba SC, Evans Aveva aliiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba walimruhusu Juuko na wanashangaa kwa nini hakwenda. “Sisi kwetu, mchezaji kuitwa timu ya taifa ni jambo la faraja, lakini tunashangaa Juuko pamoja na kumruhusu hakwenda,”.
    Vivyo hivyo, Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba amesema kwamba wao walimruhusu Brian, lakini wanashangaa hakwenda.
    “Tumerudi Dar es Salaam Jumatatu kutoka Tanga (kwenye mechi ya Ligi Kuu na Coastal Union) na tukampa ruhusa Brian kwenda kuitumikia timu ya taifa. Sasa kusikia hajaenda, inashangaza,”amesma.
    Brian Majwega aliruhusiwa akaichezee Uganda baada ya mechi na Coastal Union, lakini hakwenda

    Ushindi wa Uganda unamaanisha The Cranes sasa imeifunga Nigeria mara nne kati ya mara nane walizokutana, Super Eagles wakishinda mechi tatu na sare moja.
    Bila shaka, Wanigeria sasa wataiheshimu Uganda, ambayo iliwafunga 2-1 katika Nusu Fainali ya Kombe la Mataifa Afrika mwaka 1978 kabla ya Korongo wa Kampala kwenda kufungwa 2-0 na wenyeji Ghana kwenye fainali.
    Kikosi cha Uganda juzi kilikuwa; Denis Onyango, Joseph Nsubuga, Alex Kakuba, Shafik Bakaki, Richard Kasaga, Derrick Tekkwo/Keziron Kizito, Khalid Aucho, Godfrey Walusimbi/Robert Ssentongo, Luwagga Kizito/Ibrahim Kiyemba, Farouk Miya/Chrizestom Ntambi na Geoffrey Massa.
    Nigeria; Vincent Enyeama, Balogun, Ogbonnaya, Omeruo, Chima Akas, Sone Aluko, Ogenyi Onazi, Akpan, Ahmed Musa, Odion Ighalo na Ujah.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: JUUKO WA SIMBA AMSONONESHA MICHO, ASIKITISHWA PIA NA WINGA WA AZAM, MAJWEGA KUIPUUZA TIMU YA TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top