• HABARI MPYA

  Jumatano, Machi 25, 2015

  YANGA SC WALEEE, MSUVA YULEEE…JKT APIGWA TATU, AZAM FC, KAVUMBANGU SASA ‘WANAISOMA’

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  YANGA SC imezidi kupaa kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kufuatia ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya JKT Ruvu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Katika mchezo huo ‘mwepesi’ kwao, Yanga SC ilikwenda kupumzika ikiwa inaongoza kwa mabao 2-1, yaliyofungwa na Simon Msuva na Danny Mrwanda, dhidi ya la JKT lililofungwa na Samuel Kamuntu.  
  Msuva alifunga bao lake la 10 katika Ligi Kuu msimu huu dakika ya 33 kwa mkwaju wa penalti na kumfikia kinara wa mabao katika ligi hiyo, Didier Kavumbagu wa Azam FC.S
  Simon Msuva (kushoto) akishangilia na Danny Mrwanda baada ya kufunga

  Penalti hiyo ilitolewa baada ya beki wa JKT Ruvu, Ramadhani Haruna Shamte kuunawa mpira uliopigwa na Msuva na refa Isihaka Shirikisho wa Tanga, aliyesaidiwa na Milambo Tshikungu na Mashaka Mandembwa, wote wa Mbeya ‘akatenga tuta’.
  Danny Davis Mrwanda akaifungia bao la pili Yanga SC dakika ya 41, akimalizia krosi ya Simon Msuva. Sifa zaidi zimuendee Mrisho Khalfan Ngassa aliyepanda na mpira kwa kasi akiwapangua wachezaji wa JKT kabla ya kumpelekea mpira Msuva, aliyempasia Mrwanda akafunga.
  JKT ilipata bao lake karibu kabisa na mapumziko, mfungaji, Samuel Kamuntu aliyetumia makosa ya beki wa kulia, Juma Abdul.
  Nahodha wa Yanga SC, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alijikuta anatupiana makonde na Juma Abdul kwa kumlaumu kufanya uzembe uliosababisha JKT wapate bao.
  Mrisho Ngassa wa Yanga SC akimtoka Jabir Aziz wa JKT Ruvu
  Haruna Niyonzima akiwaacha chini mabeki wa JKT Ruvu baada ya kuwalamba 'vyenga'

  Wawili hao walianza kutoleana maneno makali uwanjani na hali hiyo ikaendelea hadi kwenye sebule ya kuelekea kwenye chumba chao cha kubadilishia nguo, ambako ndipo walipotupiana makonde.
  Ilibidi viongozi wa benchi la Ufundi la klabu hiyo wakiongoza na Meneja Hafidh Saleh wawaachanishe- na baadaye wakasuluhishwa chumbani.
  Kipindi cha pili, Yanga SC walirejea na moto wao na kufanikiwa kupata bao la tatu lililofungwa na Msuva, tena akimalizia pasi ya Ngassa. Msuva sasa ndiye anaongoza kwa mabao Ligi Kuu, 11 dhidi ya 10 ya Kavumbangu.
  Yanga SC waliendelea kutawala mchezo na kupeleka mashambulizi zaidi langoni mwa JKT, lakini hawakuwa na bahati ya mabao zaidi.
  Kwa ushindi huo, Yanga SC inafikisha pointi 40 baada ya kucheza mechi 19, moja zaidi ya mabingwa watetezi, Azam FC wenye pointi 36.
  Kikosi cha JKT Ruvu; Benjamin Haule, Damas Makwaya, Ramadhani Shamte, Renatus Morris, Mohammed Fakhi, Nashon Naftali, Amos Mgisa/Ally Bilal dk58, Jabir Aziz, Samuel Kamuntu, Iddi Mbaga/Emmanuel Pius dk41 na Alex Abel.
  Yanga SC; Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Mbuyu Twite, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Said Juma ‘Makapu’, Salume Telela, Haruna Niyonzima/Nizar Khalfan dk 87, Danny Mrwanda/Hussein Javu dk72, Mrisho Ngassa na Simon Msuva.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA SC WALEEE, MSUVA YULEEE…JKT APIGWA TATU, AZAM FC, KAVUMBANGU SASA ‘WANAISOMA’ Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top