• HABARI MPYA

  Jumapili, Machi 22, 2015

  HANS POPPE AMTAKIA KILA HERI TAMBWE YANGA, ASEMA ‘WALA HAWASHITUKI NAYE’

  Na Dina Ismail, DAR ES SALAAM
  MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili wa Simba SC, Zacharia Hans Poppe amemtakia mafanikio zaidi mshambuliaji wao wa zamani, Mrundi Amisi Joselyn Tambwe katika timu yake mpya, Yanga SC.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY leo mjini Dar es Salaam, Hans Poppe amesema kwamba hawakumuacha Tambwe kwa nia mbaya, bali walimuacha ili kumsaidia mwenyewe mchezaji huyo.
  Akifafanua, Hans Poppe alisema kwamba Tambwe alifanya vizuri wakati wa kocha Mcroatia, Zdravko Logarusic, lakini baada ya ujio wa kocha mwingine, Mzambia Patrick Phiri mambo yakageuka.
  Hans Poppe (kushoto) akiwa na Rais wa Simba SC, Evans Aveva
  Amisi Tambwe enzi zake akiichezea Simba SC

  “Katika mfumo wa Loga, Tambwe alikuwa anafunga sana mabao hadi kawa mfungaji bora Ligi Kuu, kwa sababu ya mfumo wa yule kocha. Lakini baada ya kuja Phiri, akaja na mfumo mwingine, ambao ukamfanya Tambwe aonekane hana thamani,”amesema Hans Poppe.
  Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), amesema baada ya hali hiyo, ili kumsaidia mchezaji huyo, wakazungumza wamuache akatafute timu nyingine ili kumsaidia akaokoe kipaji chake.
  “Na tulipomuacha, tena Manji (Yussuf, Mwenyekiti wa Yanga SC) akampigia Rais wetu (Evans Aveva) kuomba kumsajili. Rais akamuambia hakuna shida. Wakamsajili,”amesema Poppe.
  Kwa sasa huduma ya Tambwe inapatikana Yanga SC

  Hata hivyo, Poppe ambaye alikuwa miongoni mwa askari wa JWTZ waliopigana vita ya Kagera dhidi ya majeshi ya rais wa zamani wa Uganda Nduli Iddi Amin Dada (sasa marehemu), amesema Tambwe ameanza kung’ara Yanga SC baada ya makocha wa klabu hiyo kubadili mfumo.
  “Mwanzoni Yanga walikuwa wanatumia mfumo wa mawinga, viungo wachache. Kwa hiyo ikawa vigumu kwa Tambwe kung’ara. Lakini kwa sasa, wanatumia viungo wengi, naye anafanya vizuri,”amesema.
  Poppe amesema hawana kabisa kinyongo na Tambwe na pamoja na kumshukuru kwa mchango wake alipokuwa kwao, pia wanamtakia kila la heri katika maisha yake mapya kwa mahasimu, Yanga SC.
  Hadi sasa, Tambwe tayari amefunga mabao saba katika mechi 16 tangu atue Yanga SC Desemba akitokea kwa mahasimu Simba SC, waliomsajili msimu uliopita kutoka Vital’O ya Burundi.
  Simba SC ilimsajili Tambwe baada ya kuvutiwa naye kwa kuwa mfungaji bora wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati mwaka juzi nchini Sudan, akiiwezesha na Vita’O kutwaa taji la kwanza la michuano hiyo maarufu kama Kombe la Kagame.
  Simba SC ikanufaika na mabao ya Tambwe katika msimu uliopita wa Ligi Kuu akiibuka pia mfungaji bora wa higi hiyo.
  Hadi anaachwa Desemba, Tambwe alikuwa ameifungia Simba SC jumla ya mabao 26 katika mechi 43.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: HANS POPPE AMTAKIA KILA HERI TAMBWE YANGA, ASEMA ‘WALA HAWASHITUKI NAYE’ Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top