• HABARI MPYA

  Jumanne, Machi 31, 2015

  SAMATTA: WASHAMBULIAJI WENGI STARS, WANAMCHANGANYA KOCHA

  Na Mahmoud Zubeiry, MWANZA
  MSHAMBULIAJI wa TP Mazembe ya DRC, Mbwana Ally Samatta amesema kwamba timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ina washambuliaji wengi kiasi kwamba inamchanganya kocha katika kupanga kikosi. 
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY juzi mjini hapa baada ya mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Malawi, Samatta alisema kwamba ni jambo zuri timu kuwa na wachezaji wengi, lakini inafikia wakati kocha anapagawa amuanzishe yupi.
  Hata hivyo, Samatta amesema hiyo ni nzuri kwa sababu inapotokea kocha akatoa mchezaji, hata anayeingia yuko vizuri na anakwenda kuisaidia timu.
  Mbwana Samatta aliifungia bao la kusawazisha Taifa Stars ikitoka sare ya 1-1 na Malawi Jumapili
  Samatta akimtoka beki wa Malawi CCM Kirumba juzi


  Katika mchezo wa juzi Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Stars iliponea chupuchupu kufungwa kama si Samatta kusawazisha bao dakika ya 76 akiwa katikati ya mabeki wawili wa The Flames, baada ya kupewa pasi nzuri na kiungo wa Yanga SC, Mrisho Khalfan Ngassa.   
  Esau Kanyenda alianza kuifungia Malawi dakika ya tatu tu ya mchezo, baada ya kuuwahi mpira uliorudi kufuatia kona ya Haray Nyirenda kuzua kizaa langoni mwa Taifa Stars.
  Samatta amesema Taifa Stars kwa sasa iko vizuri na kuna vitu vimeongezeka kwenye maeneo kadhaa, kutokana na vijana wadogo kuongezwa kikosini, kwani hiyo imeongeza chachu na hali ya watu kujituma. 
  “Kuna vitu vimeongezeka japo si vikubwa kutoka kwa wachezaji wapya. Malawi ni timu ambayo tunafahamiana vizuri, michezo mingi tunacheza na Malawi sijashangaa matokeo kama haya, kwa sababu wamekwishatuzoea.
  Baadhi ya vijana wadogo walioongeza chachu katika kikosi cha Taifa Stars, Juma Luizio kulia na Said Ndemla kushoto juzi waliketi jukwaani kabisa Kirumba
  “Mechi za kufahamiana siku zote zinakuwa ngumu, hata kama tungecheza kwao, nao ingekuwa tabu vile vile kwao. Kwa viwango hatujatofautiana sana. Popote ambako tungecheza, matokeo ya droo yasingekuwa ya kustaajabisha,”amesema Samatta.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SAMATTA: WASHAMBULIAJI WENGI STARS, WANAMCHANGANYA KOCHA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top