• HABARI MPYA

    Saturday, March 07, 2015

    MFUMO ULE ULE, GORAN NA PLUIJM UWEZO NA JUHUDI ZA WACHEZAJI NDIVYO VITAAMUA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    NYASI za Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kesho zinatarajiwa kuwaka moto kwa mchezo wa mahasimu wa jadi katika soka ya Tanzania, Simba SC dhidi ya Yanga SC.
    Simba SC ‘inayoishi’ Mtaa wa Msimbazi, jirani kabisa na kwa mahasimu wao, Jangwani eneo la Kariakoo, Dar es Salaam, imekuwa kambini visiwani Zanzibar kwa wiki yote hii kujiandaa na mchezo huo wa marudiano Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Yanga SC, yenyewe baada tu ya kurejea kutoka Botswana ilipokwenda kuchukua tiketi ya kusonga mbele Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuitoa BDF ya huko, ilikwenda kujichimbia Bagamoyo kwa maandalizi ya mchezo huo.
    Kiungo wa Yanga SC akikabiliana na beki wa Simba SC, Juuko Murushid katika mchezo uliopita wa Nani Mtani Jembe 

    Ni kawaida, unapowadia mchezo wa watani, hata mechi hiyo irudi mara nne kwa mwaka, lakini lazima timu hizo zitahitaji kambi ya nje ya mji kwa maandalizi.
    Gumzo kubwa kwa sasa katika vijiwe vya wapenda soka nchini ni kuhusu mchezo huo, mashabiki wa timu zote mbili wakitambiana kila upande ukiamini utaibuka na ushindi.
    Na katika tambo hizo silaha ni wachezaji- Simba wanatambia nyota wao wakiongozwa na Mganda Emanuel Okwi na Yanga SC nao wanatambia wakali wao, wakiongozwa na Mrundi, Amisi Tambwe.
    Okwi na Tambwe wanatajwa zaidi katika mijadala ya kuelekea mchezo huo, kwa kuwa ni wachezaji ambao wameonyesha kiu ya kufanya kitu katika soka ya Tanzania.
    Tambwe ni mchezaji aliyekuwa Simba SC msimu uliopita na Okwi alikuwa Yanga SC msimu huo. Wote waliachwa na klabu zao na kwa bahati nzuri wapinzani wakawachukua.
    Wote wana ‘hasira’ za kuwathibitishia mabosi wao wa zamani walifanya makosa kuwaacha na kwa sababu hiyo, Okwi na Tambwe ndiyo wachezaji wanaotarajiwa kutazamwa zaidi hiyo kesho.
    Emmanuel Okwi anatarajiwa kuendelea kuwa mwiba kwa safu ya ulinzi ya Yanga SC

    Bado kila timu ina wakali wengine kikosini ambao wanaweza kung’ara katika mchezo wa kesho. 
    Pale Simba SC wapo Mganda mwingine, Danny Sserunkuma na wazalendo kama Ramadhani Singano ‘Messi’, Ibrahim Hajib na Elias Maguri, wakati Yanga SC kuna Mliberia Kpah Sherman na wazalendo Mrisho Ngassa, Simon Msuva na Danny Mrwanda.
    Ukitazama mechi za karibuni za timu hizo, utagundua timu zote zinatumia aina moja ya mchezo- mabeki wanne, viungo wawili, mawinga wawili na washambuliaji wawili- mfumo fulani wa 4-4-2 na wote wakishambulia zaidi kutokea pembeni.     
    Kikosi cha Simba SC kesho kama si Peter Manyika langoni, basi atakuwa Ivo Mapunda ambaye atalindwa na mabeki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Hassan Kessy, Hassan Isihaka na Juuko Murushid au Joseph Owino, wote Waganda.
    Kiungo mkabaji kama kawaida Jonas Mkude, juu yake mchezeshaji Said Ndemla wakati Ramadhani  Singano na Emmanuel Okwi watakuwa wanashambulia kutokea pembeni.
    Washambuliaji gani wataanza kwa Simba SC kesho? Hilo ndilo swali. Hakuna shaka Dan Sseunkuma ataanza, lakini pacha wake mbele anaweza akawa Elias Maguri au Ibrahim Hajib.
    Hajib anapewa nafasi kubwa ya kuanza kesho kwa kuwa yuko katika ubora hivi sasa, akitoka kufunga mabao matatu katika ushindi wa 5-0 dhidi ya Prisons Jumamosi iliyopita.
    Na ni mchezaji anayewatia homa mahasimu Yanga SC, ambao wiki yote hii wamekuwa wakipinga kuchezeshwa dhidi ya Prisons akiwa ana kadi tatu za njano.
    Simba SC ilitumia kanuni mpya za Ligi Kuu, kumuombea mchezaji huyo acheze mechi dhidi ya Prisons na Yanga SC licha ya kuwa na kadi tatu za njano, ilia aje kukosa mechi za baadaye.
    Hata hivyo, Yanga SC wamekuwa wakiishambulia Bodi ya Ligi Kuu wiki yote hii kwa kumruhusu mchezaji huyo kucheza. Maana yake nini, wanamugopa?
    Kwa Yanga SC pale, kama si Deo Munishi ‘Dida’ langoni atasimama Ally Mustafa ‘Barthez’, mabeki Mbuyu Twite au Juma Abdul, Oscar Joshua au Edward Charles kwa pembeni na katikati Nadir Cannavaro na Kevin Yondan au Rajab Zahir.
    Kiungo mkabaji Salum Telela na mchezeshaji Haruna Niyonzima wakati mawinga wanaweza kuwa Simon Msuva na Mrisho Ngassa, huku Amisi  Tambwe na Danny Mrwanda au Kpah Sherman wakicheza mbele ya lango ‘la adui’.
    Mchezo unaweza sana ‘kubalansi’ iwapo makocha watarudi na mipango ile ile tuliyoishuhudia siku za karibuni katika mechi zao, zaidi sasa uwezo na juhudi za wachezaji ndivyo vitaleta vitu vya ziada uwanjani.
    Wachezaji wa Simba SC wamekuwa wakijtuma sana inapowadia mechi dhidi ya Yanga SC- bila shaka wanajua wanapofaya vizuri katika mchezo huo kuna posho nzuri.
    Wachezaji wa Yanga SC wamekuwa ‘wepesi’ mno kwenye mchezo dhidi ya mahasimu wao na wataingia uwanjani kesho wakiwa na kumbukumbu ya kipigo cha mabao 2-0 katika mechi ya Mtani Jembe Desemba 13 mwaka jana. 
    Yanga SC ya ‘siku hizi’ inaweza kushinda mechi ngumu, lakini hata wakikutana na Simba dhaifu kiasi gani, matokeo mazuri yamekuwa sare.
    Lakini ikumbukwe, mchezo huu ni wa kwanza kuwakutanisha Mholanzi Hans van der Pluijm na Mserbia Goran Kponovic wakiwa na Simba na Yanga.
    Kikosi cha Simba SC katika mechi za karibuni
    Kikosi cha Yanga SC katika mechi za karibuni

    Pluijm aliifundisha Yanga SC msimu uliopita na alikutana na Simba SC katika mchezo mmoja tu, akatoa sare ya 1-1, tena timu yake ikisawazisha dakika ya 86 kupitia kwa Simon Msuva, baada ya Haroun Chanongo kutangulia kuwafungia Wekundu wa Msimbazi dakika ya 76. 
    Lakini makocha wasaidizi wa timu zote, Charles Boniface Mkwasa wa Yanga SC na Suleiman Matola wa Simba SC wote ni wazoefu wa mechi za watani kwa kuanzia kuzicheza wakiwa wachezaji.
    Yanga SC wanaingia kwenye mchezo wa kesho wakihitaji pointi ili kujiimarisha kileleni, wakati Simba SC inahitaji pointi za kuwarudisha kwenye mbio za ubingwa. Patamu hapo!
    Isipokuwa tu, timu zote zinaonekana kucheza mfumo wa aina moja, maana yake jitihada za wachezaji ndizo zitasababisha matokeo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MFUMO ULE ULE, GORAN NA PLUIJM UWEZO NA JUHUDI ZA WACHEZAJI NDIVYO VITAAMUA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top