• HABARI MPYA

    Thursday, October 16, 2014

    NIYONZIMA HATARINI KUWAKOSA SIMBA SC JUMAMOSI, AUMIA ENKA…JAJA, CANNAVARO NA YONDAN NAO BADO ‘MDOGO MDOGO’

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    KIUNGO wa Yanga SC, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima yuko kwenye hatihati ya kuikosa mechi dhidi ya watani wa jadi, Simba SC keshokutwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Hiyo inafuatia kuumia enka katika mazoezi ya jana Uwanja wa Boko Veterani na kutolewa nje, akiwa amefungwa barafu.
    Si daktari wa Yanga, Sufiani Juma au kocha Mkuu, Marcio Maximo aliyekuwa tayari kuzungumzia hali ya kiungo huyo wa kimataifa wa Rwanda, lakini sura ya Nahodha huyo wa Amavubi ilionyesha anakabiliwa na maumivu.
    Haruna Niyonzima akiwa amefungwa kifundo chake cha mguu wa kulia baada ya kuumia jana. Hapa anawaangali wenzake wakiendelea na mazoezi

    Niyo anaungana na wachezaji wengine watatu ambao wapo kwenye hatihati ya kucheza mechi hiyo, mabeki Nadir Haroub Ali ‘Cannavaro’ na Kevin Patrick Yondan pamoja na mshambuliaji Mbrazil, Genilson Santana Santos ‘Jaja’.
    Watatu hao wote jana walikuwa wanafanya mazoezi mepesi na kama leo pia hawataweza kujumuika na wenzao, ina maana kuanza keshokutwa itakuwa nadra.
    Lakini wachezaji wengine wote wa Yanga SC wapo vizuri kuelekea mchezo huo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Yanga SC imeweka kambi katika hoteli ya Landmark, Kunduchi, Dar es Salaam wakati mahasimu wao wamerejea leo kutoka Johannesburg, Afrika Kusini walipokuwa wameweka kambi tangu Oktoba 8, mwaka huu.  
    Nadir Cannavaro kulia, Kevin Yondan katikati na Genilson Jaja kushoto wakifanya mazoezi mepesi ya peke yao jana
    Kocha Marcio Maximo akitoa maelekezo kwa kiungo Hassan Dilunga mazoezini jana
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NIYONZIMA HATARINI KUWAKOSA SIMBA SC JUMAMOSI, AUMIA ENKA…JAJA, CANNAVARO NA YONDAN NAO BADO ‘MDOGO MDOGO’ Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top