• HABARI MPYA

    Friday, February 07, 2014

    KAZE SASA FITI, KUREJEA UWANJANI SIMBA NA MGAMBO

    Na Baby Akwitende, Dar es Salaam 
    BEKI wa kimataifa wa Simba kutoka nchini Burundi, Gilbert Kaze, anatarajiwa kurejea uwanjani Jumapili katika mechi ya Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara dhidi ya JKT Mgambo itakayofanyika kwenye uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
    Kaze alikuwa na maumivu kwenye goti na amekaa nje katika mechi mbili zilizopita ambazo Simba ilikutana na JKT Oljoro na Jumatano ilipoikabili Mtibwa Sugar kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY leo asubuhi, Kocha Msaidizi wa Simba, Suleiman Matola, alisema kwamba Kaze ameshapona na alianza mazoezi mepesi na wachezaji wenzake wakati timu ilipokuwa mkoani Morogoro.
    Kifaa kimerudi; Kaze Gilbert amepona na atarejea uwanjani Jumapili

    Matola alisema kuwa wamefurahi kurejea kwa beki huyo wa kati katika kikosi chao na wanaamini sasa safu yao ya ulinzi itazidi kuimarika.
    “Unapokuwa na mchezaji majeruhi, mnapata tabu kujua nani aanze na nani asubiri benchi, lakini wachezaji wanapokuwa inakuwa ni furaha kwa benchi na maamuzi ya kupata kikosi cha kwanza yanakuwa mepesi,” alisema kiungo huyo wa zamani wa Simba.
    Alimtaja beki wa pembeni, Nassor Masoud ‘Chollo’ ndiye mchezaji pekee majeruhi  katika kikosi hicho kilichoko katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ya Bara inayoshirikisha klabu 14 za hapa nchini.
    Simba SC tayari ipo Tanga kwa ajili ya mchezo wao ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, dhidi ya Mgambo JKT Jumapili Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.  
    Mwisho….

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KAZE SASA FITI, KUREJEA UWANJANI SIMBA NA MGAMBO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top