• HABARI MPYA

    Friday, November 15, 2013

    MKWASA AMUONYA DILUNGA; “USIPOKUWA MAKINI YANGA, UTAPOTEA KWENYE RAMANI NDANI YA MUDA MFUPI SANA”

    Na Mahmoud Zubeiry, Ilala
    KOCHA Mkuu wa Ruvu Shooting ya Pwani, Charles Boniface Mkwasa amempongeza kiungo wake chipukizi, Hassan Dilunga kusaini Yanga SC, lakini amemuambia asipokuwa makini atapotea ndani ya muda mfupi tu kwenye ramani ya soka.  
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY usiku huu, Mkwasa amesema kwamba Dilunga ni mchezaji mzuri na amekuwa tegemeo lake Ruvu Shooting, hivyo kwenda kwake Yanga ni pigo kwa timu yake.
    Usipokuwa makini, utapotea haraka; Hassa Dilunga akiichezea Ruvu Shooting

    Wosia; Charles Boniface Mkwasa amemuasa Dilunga akazane kugombea namba Yanga vinginevyo atapotea haraka
    “Ni mchezaji ambaye tumekuwa naye tangu akiwa mdogo, tumemlea vizuri hapa hadi amekuwa tegemeo la timu. Kwa kweli nafurahia mafanikio yake, kwanza kuitwa Stars (timu ya taifa) na pia kusajiliwa Yanga.
    Yanga ni timu kubwa, wazi atapata maslahi mazuri, lakini anatakiwa akazane katika mazoezi ili awe fiti zaidi na kuweza kugombea namba pale Yanga, kwa sababu kuna wachezaji wazuri sana wa nafasi yake,”alisema.
    Mkwasa alisema iwapo Dilunga hatajibidiisha katika mazoezi na kujikuta anakosa namba katika kikosi cha kwanza Yanga, maana yake atapoteza nafasi Taifa Stars na mwisho wa siku klabu hiyo pia itamtoa kwa mkopo na huo ndiyo ukawa mwisho wake kisoka.   
    Dilunga kushoto akikabiliana na mmoja wa viungo wa Yanga, Haruna Niyonzima kulia anayepasua katikati ya wachezaji wa Ruvu
    Dilunga katika picha tofauti akiichezea Ruvu Shooting

    “Kwa kweli Dilunga asipokuwa makini atapotea ndani ya muda mfupi. Bado kijana mdogo na kusajiliwa Yanga ni nafasi nzuri kwake kukuza kipaji chake, ila lazima ajitambue na atambue changamoto zinazomkabili,”alisema.
    Dilunga anaingia kwenye orodha ya viungo kibao na wote mafundi waliopo Yanga SC, akina Athumani Iddi ‘Chuji’, Frank Domayo ambao pia ni wapinzani wake wa namba Taifa Stars, Nizar Khalfan, Haruna Niyonzima, Salum Telela na Hamisi Thabit.  
    Kiungo huyo amesaini jana usiku Mkataba wa miaka mitatu na Yanga, ingawa uongozi wa Ruvu Shooting umekaririwa leo ukisema, bado ana Mkataba pia na timu hiyo ya jeshi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MKWASA AMUONYA DILUNGA; “USIPOKUWA MAKINI YANGA, UTAPOTEA KWENYE RAMANI NDANI YA MUDA MFUPI SANA” Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top