• HABARI MPYA

  Saturday, April 14, 2018

  MTIBWA SUGAR YAMPA MKATABA MPYA MCHEZAJI MWINGINE CHIPUKIZI WA NGORONGORO HEROES

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KLABU ya Mtibwa Sugar imeendeleza sera zake za kulea vipaji vya wanasoka chipukizi, baada ya kumsainisha mkataba mpya wa miaka miwili, beki wa kulia, Kibwana Ally Shomary.
  Katibu Msaidizi wa Mtibwa Sugar, Abubakar Swabur ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo kwamba Shomary amesaini mkataba huo mpya kufuatia mkataba wake wa awali wa miaka miwili pia kukaribia kumalizika.
  Mchezaji huyo, zao la timu ya vijana ya Mtibwa Sugar msimu huu amecheza mechi mbili za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara katika kikosi cha kwanza na zote amefanya vizuri.
  Beki chipukizi wa kulia, Kibwana Ally Shomary baada ya kusaini mkataba mpya Mtibwa Sugar
  Kkutoka kushoto Katibu Msaidizi wa Mtibwa Sugar, Abubakar Swabur, Kibwana Shomary na kaka yake, Nestory 
  Mechi hizo nidhidi ya Singida United timu hiyo ikishinda 3-0 Uwanja wa Namfua na dhidi ya Simba SC Jumatatu wiki hii Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro timu hiyo ikichapwa 1-0.
  Swabur amesema kwamba Shomary alisimamiwa na kaka yake aliyemtambulisha kwa jina la Nestory wakati wa kusaini mkataba huo.
  Huyo anakuwa kinda wa pili kupewa Mtibwa Sugar ndani ya wiki tatu, kufuatia mwingine, Dickson Job ambaye naye alisaini mkataba mpya wa miaka mitatu kuendelea kuichezea timu hiyo.
  Wawili hao, wote ni wachezaji wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes ambao walikuwamo kwenye kikosi cha timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys kilichoshiriki fainali za Afrika (AFCON U17) nchini Gabon Mei mwaka jana.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MTIBWA SUGAR YAMPA MKATABA MPYA MCHEZAJI MWINGINE CHIPUKIZI WA NGORONGORO HEROES Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top