• HABARI MPYA

    Saturday, March 03, 2018

    RAZACK ABALORA ASIMAMISHWA ETI ALIMTUKANA REFA MECHI NA SIMBA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KAMATI ya Bodi ya Ligi ya Uendeshaji na Usimamizi ya Ligi imemsimamisha kipa wa Azam FC, Razack Abalora hadi suala lake litakapotolewa uamuzi na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
    Kwa mujibu wa barua kutoka bodi hiyo iliyotumwa jana saa 4 usiku, inaeleza kuwa Abalora anasimamishwa akidaiwa kumtolea lugha chafu mwamuzi Jonesia Rukyaa, mara baada ya kumalizika kwa mchezo dhidi ya Simba uliofanyika Februari 7 mwaka huu.
    “Katika mechi namba 135 dhidi ya Simba iliyochezwa Februari 7, 2018 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, mchezaji wako Razack Abalora alimtolea lugha chafu mwamuzi (Jonesia Rukyaa) baada ya filimbi ya mwisho,” ilieleza sehemu ya nukuu ya barua hiyo.
    Razack Abalora amesimamishwa hadi suala lake litakapotolewa uamuzi na Kamati ya Nidhamu ya TFF

    Aidha barua hiyo iliyoandikwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa bodi hiyo, Boniface Wambura, iliendelea kueleza kuwa: “Kwa vile suala lake ni la kinidhamu, na kwa kutumia Kanuni ya 9(5) ya Ligi Kuu, Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imemsimamisha kucheza mechi za Ligi Kuu hadi suala lake litakaposikilizwa na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).”
    Barua hiyo ilimalizia kuwa, Abalora aliyesajiliwa akitokea WAFA FC ya Ghana atafahamishwa siku ya kikao cha kamati hiyo kusikiliza shauri lake ambapo pia ataruhusiwa kuwasilisha utetezi wake.
    Kusimamishwa kwa Abalora kunakuja baada ya kupita takribani mwezi mmoja huku mchezaji akiwa ameshacheza mechi takribani nne, jambo ambalo linaweka viulizo kwanini asimishwe hivi sasa na sio siku chache baada ya kutenda kosa hilo.
    Uamuzi hii wa aina hii haupo kabisa kwenye soka la kisasa kwa vyombo vya uendeshaji wa ligi, mara kwa mara tumeshuhudia katika ligi za wenzetu wakichukua hatua kwa haraka ndani ya siku kadhaa kwa wachezaji wanaofanya vitendo vya utovu wa nidhamu.
    Kinyume na uweledi wanaofanya wenzetu, soka la Tanzania bado limekuwa na uamuzi wa kianalojia yaani uamuzi unaweza kuchukulia hata baada ya mwezi na zaidi kupita, hii hupelekea uamuzi mwingi kuwa na viulizo licha ya kuundwa kwa vyombo vya kusimamia ligi ambavyo viliundwa kwa kazi yakushughulikia mambo hayo kwa uharaka.
    Azam FC inaheshimu uwepo wa vyombo hivi, lakini tunachoomba ni lazima vifanye kazi yao kwa uharaka ili kuondoa viulizo kwenye maamuzi wanayochukua baada ya muda mrefu kupita tena taarifa nyingine zikitumwa usiku siku moja kabla kuelekea mchezo husika wa klabu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: RAZACK ABALORA ASIMAMISHWA ETI ALIMTUKANA REFA MECHI NA SIMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top