• HABARI MPYA

    Thursday, March 08, 2018

    MAYANGA AMBEBA KABWILI STARS, AMTEMA MANYIKA KIKOSI KITAKACHOCHEZA NA ALGERIA NA DRC

    Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
    KOCHA Mkuu wa timu ya taifa ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, Salum Mayanga ameteua wachezaji 23 kwa ajili ya michezo miwili ya kujipima nguvu dhidi ya timu za Algeria na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) mwezi huu, safari hii akimuacha kipa Peter Manyika wa Singida United na kumchukua kinda, Ramadhani Kabwili wa Yanga SC.
    Katika mkutano na Waandishi wa Habari leo makao makuu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Mayanga amewaita kikosini wachezaji wote wanaocheza nje, akiwemo Nahodha mshambuliaji Mbwana Ally Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji.
    Amewaita pia Simon Msuva wa Difaa Hassan El Jadida ya Morocco, Hamisi Abdallah wa Tusker FC ya Kenya, Farid Mussa CD Teneriffe B ya Hispania na Thomas Ulimwengu ambaye hana timu kwa sasa.
    Kipa kijana mdogo wa Yanga SC, Ramadhani Kabwili ameitwa Taifa Stars huku Peter Manyika wa Singida United akiachwa 

    Kikosi kamili cha Taifa Stars ni; Makipa; Aishi Manula (Simba SC), Abdulrahman Mohammed (JKU), Ramadhan Kabwili (Yanga SC), mabeki; Shomary Kapombe (Simba SC), Hassan Kessy (Yanga SC), Gardiel Michael (Yanga SC), Kelvin Yondan (Yanga SC), Abdi Banda (Baroka FC/Afrika Kusini), Erasto Nyoni (Simba SC).
    Viungo ni Hamisi Abdallah (Tusker/Kenya), Mudathir Yahya (Singida United), Said Ndemla (Simba SC), Faisal Salum (JKU), Abdulaziz Makame (Taifa Jangombe), Farid Mussa (CD Teneriffe B/Hispania), Thomas Ulimwengu (Huru), Ibrahim Ajib (Yanga SC), Shiza Kichuya (Simba SC),na Mohammed Issa ‘Banka’ (Mtibwa Sugar).
    Washambuliaji ni Mbwana Samatta (KRC Genk/Ubelgiji), Simon Msuva (Difaa Hassan El Jadida/Morocco), John Bocco (Simba SC) na Yahya Zayed (Azam FC) na kikosi kinatarajiwa kuingia kambini Machi 18 mwaka huu kwenye hoteli ya SeaScape iliyopo Kunduchi mjini Dar es Salaam kabla ya kwenda Algeria Machi 19.
    Taifa Stars inatarajia kucheza michezo miwili ya kirafiki iliyo katika kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) mwezi huu, ikianzia ugenini nchini Algeria Machi 22 dhidi ya wenyeji, The Greens kabla ya kurejea nyumbani, Dar es Salaam kuwakaribisha The Leopards Machi 27 Uwanja wa Taifa.
    Mara ya mwisho Taifa Stars iliteremka uwanjani Novemba 1 na kulazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na wenyeji, Benin katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa l'Amitie, au Urafiki mjini Cotonou.
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na marefa wa nchini humo, Ligali Praphiou aliyesaidiwa na Bello Razack na Koutou Narcisse, hadi mapumziko wenyeji The Squirrels, walikuwa mbele kwa bao 1-0.
    Bao hilo lilifungwa dakika ya 33 kwa penalti na mkongwe mwenye umri wa miaka 33, Nahodha, Stephane Sessegnon anayechezea klabu ya Montpellier ya Ufaransa.
    Hata hivyo, ilikuwa ni penalti ya mashaka, kwani mchezaji aliyeugusa mpira huo kwa mkono alikuwa ni wa Benin, Khaled Adenon lakini refa akadhani ni mchezaji wa Tanzania.
    Sessegnon akamtungua kipa namba moja wa Tanzania, Aishi Manula kufunga bao lake la 21 timu ya taifa katika mechi ya 68.
    Wachezaji wa Tanzania wakamlalamikia refa kwa kutowapa penalti dakika ya 32 kufuatia, winga Simon Msuva kuangushwa kwenye boksi baada ya kusukumwa.
    Kipindi cha pili, Tanzania ilikianza kwa nguvu na kasi zaidi wakishambulia kutokea pembeni na hatimaye kufanikiwa kupata bao la kusawazisha.
    Alikuwa ni mshambuliaji wa zamani wa Simba ya Tanzania na Dhofar SC ya Oman, Elias Maguri aliyefunga bao hilo akimalizia krosi ya winga Shiza Kichuya kutoka upande wa kushoto dakika ya 50.
    Matokeo haya yanamaanisha Benin ilishindwa kulipa kisasi kwa Tanzania, kwani mara ya mwisho, zilipokutana Oktoba 12, mwaka 2014 Taifa Stars ilishinda 4-1, mabao ya Nahodha wa wakati huo, beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ dakika ya 16, kiungo Amri Kiemba dakika ya 39, Thomas Ulimwengu dakika ya 49 na Juma Luizio, wakati la Benin lilifungwa na Suanon Fadel dakika ya 90.
    Kwa sasa Tanzania inashika nafasi ya 146 kwenye viwango vya FIFA, wakati DRC ni ya 39 na Algeria ni ya 60.   
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAYANGA AMBEBA KABWILI STARS, AMTEMA MANYIKA KIKOSI KITAKACHOCHEZA NA ALGERIA NA DRC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top