• HABARI MPYA

    Sunday, March 11, 2018

    KWA SABABU ZIPI VIONGOZI YANGA WAENDELEE KUWA MADARAKANI IKIWA WAMESHINDWA WAZI WAZI

    HALI ya kiuchumi ndani ya klabu ya Yanga si nzuri na imefikia wachezaji wanakaa hadi miezi mitatu au zaidi bila kulipwa mishahara, wakati pia inadaiwa Maofisa wa Sekretarieti na benchi la Ufundi wana zaidi ya nusu mwaka bila malipo.
    Kudhoofu kwa hali ya kiuchumi katika klabu kumechangia kudhoofisha na timu pia, Yanga ya sasa ikionekana kupoteza makali yake iliyokuwa nayo hadi msimu uliopita. 
    Imefikia hadi inafungwa nyumbani na timu za kawaida tu katika michuano ya Afrika kama Township Rollers ya Botswana, wakati Ligi Kuu japo ipo nafasi ya pili, ikizidiwa pointi tatu na mahasimu, Simba lakini mwenendo na kiwango cha timu kwa ujumla haviridhishi.
    Hakuna morali ndani ya timu kuanzia kwa Maofisa wa Sekretarieti, Benchi la Ufundi na hata wachezaji, kutokana na ukweli kwamba kila mmoja hafurahii kazi.
    Lakini wakati ikithibitika kwamba wachezaji wanafikisha miezi mitatu na Maofisa wengine miezi hadi sita bila kulipwa – inafahamika klabu ya Yanga ina wadhamini wasiopungua watatu.
    Hao ni wadhamini wakuu, SportPesa ambao wanatoa Sh. Bilioni 1 kwa mwaka, Macron wanaotoa Sh. Milioni 700 kasoro kidogo kwa mwaka na Maji ya Afya, ambayo haijulikani wanatoa kiasi gani kwa sababu uongozi chini ya Kaimu Mwenyekiti wake, Clement Sanga haujawahi kuweka wazi.
    Pamoja na hayo, Yanga ina mgawo kutoka kwa wadhamini wawili wa Ligi Kuu, Vodacom Tanzania na Azam TV kwa pamoja wanatoa zaidi ya Sh. Milioni 500 kwa mwaka. Yanga pia inapata fedha kutokana na udhamini wa Azam TV katika michuano ya Azam Sports Federation.
    Lakini pia, wadau, wapenzi na mashabiki wa timu bado nao wamekuwa wakichangishana fedha ili kuisaidia timu kupitia vikundi na umoja tofauti.
    Pamoja na yote, bado wachezaji wanaishi miezi mitatu na Maofisa wengine wanakaa hadi nusu mwaka bila malipo yoyote.
    Uongozi wa Yanga chini ya Kaimu Mwenyekiti, Sanga unaonekana kukosa kabisa suluhisho la matatizo zaidi tu ya kueneza propaganda za eti aliyekuwa Mwenyekiti, Yussuf Manji atarejea.
    Vyema Manji akirejea Yanga hata sasa, lakini basi uongozi wa Yanga uwaambie wanachama suluhisho la tatizo yanayoikabili kwa sasa.
    Wakati huo huo, ukifuatilia uendeshwaji wa timu tangu kuondoka kwa Manji matatizo ni mengi yote si kwa sababu ya fedha, bali uongozi tu uliokosa umakini katika utendaji wake.
    Baada ya kosa la bahati mbaya la kuwapa mikataba mipya washambuliaji majeruhi, Donald Ngoma na Amissi Tambwe na kumuongezea mkataba mshambuliaji ‘asiyejielewa’ Matheo Anthony ilitarajiwa klabu ingesajili washambuliaji wapya japo wawili mahiri katika dirisha dogo.
    Badala yake akasajiliwa chipukizi asiye na uzoefu kabisa wa Ligi, Yohanna Nkomola pekee ambaye naye kwa sasa yuko nje kwa sababu ya maumivu. Halikuwa kosa kumsajili Nkomola, lakini ilitakiwa wasajiliwe na wazoefu wawili.
    Baada ya kushindwa kumuongezea mkataba beki wa kati Mtogo, Vincent Bossou mwishoni mwa msimu uliopita, ilitarajiwa katika dirisha dogo klabu ingesajili sentahafu mwingine mahiri, lakini likasajiliwa jina tu la Mkongo, Fiston 'Festo' Kayembe Kanku yeye mwenyewe hadi leo hajaonekana.
    Sasa klabu inalazimika kutumia wachezaji wa nafasi nyingine, akiwemo kiungo Said Juma ‘Makapu’ katika nafasi ya ulinzi wa kati.
    Klabu imembebesha majukumu mazito ya Utendaji Mkuu wa klabu, kocha Charles Boniface Mkwasa bila sababu za lazima, matokeo yake ni wazi mchezaji na kocha huyo wa zamani wa timu ameelemewa. 
    Yanga ina watu wengi wa kufanya kazi za Utendaji Mkuu wa klabu na Mkwasa akaachiwa Idara yake ya Ufundi, ambako angetumika kwa ufanisi zaidi.
    Ufike wakati makundi ya wanachama na wapenzi wa Yanga waache kutetea mapungufu ya uongozi kwa kuamini ndiyo wanaifanyia wema klabu yao, kumbe wanaikandamiza.
    Viongozi wabovu ndio wameifikisha Yanga hapa ilipo, ina zaidi ya miaka 80 ikiwa haina cha kujivunia na bado hadi leo wanataka waendelee kuitumia kwa maslahi yao binafsi.
    Wanachama na wapenzi wa Yanga wawaulize viongozi wao, kwa nini klabu inakabiliwa na maradhi ya kiuchumi wakati ina wadhamini zaidi ya watatu?
    Ni ukatili mkubwa kuwafanyisha kazi watoto wa watu akina Ramadhani Kabwili, Said Mussa, Juma Mahadhi, Yussuf Mhilu bila kuwalipa mishahara kwa miezi mitatu na kiongozi wa ina hiyo anapaswa kujitathmini mara mbili anafaa vipi kuendelea kuongoza Yanga.
    Kazi ya soka ina changamoto nyingi na zaidi ni chungu na kwa mara nyingi haina mustakabali mzuri kwa wengi – yote hayo kiongozi ameshindwa kuyafikiria katika hali ya kibinadamu na bado anamtumikisha mwanaume mwenzake, mtoto wa mwanaume mwenzake bila kumlipa. Ni dhambi kubwa. 
    Na bado kiongozi anakwenda kwenye vyombo vya Habari anasema eti wamekwishawaambia wachezaji hali ya klabu ni mbaya. Inasikitisha. Watu wa aina hii kwa sababu zipi wanaendelea kuwa viongozi wa klabu ikiwa wameshindwa wazi wazi? 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KWA SABABU ZIPI VIONGOZI YANGA WAENDELEE KUWA MADARAKANI IKIWA WAMESHINDWA WAZI WAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top