• HABARI MPYA

    Saturday, February 03, 2018

    AZAM FC YARUDI NAFASI YA PILI LIGI KUU BAADA YA KUIPIGA NDANDA 3-1 CHAMAZI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    TIMU ya Azam FC imerudi katika nafasi ya pili baada ya kuichapa Ndanda FC ya Mtwara 3-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara usiku wa leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    Azam FC inafikisha pointi 33 baada ya mechi 16 za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), ikizidiwa pointi mbili na vinara Simba SC, ambao kesho wanacheza mechi yao ya 16 dhidi ya Ruvu Shooting Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Shukrani kwa mabao matatu ya nguvu yaliyofungwa na washambuliaji Yahya Zayed, Shaaban Idd na winga Enock Atta, yaliyoizamisha kabisa Ndanda, ambayo ilionyesha upinzani mkali katika mchezo huo.

    Iliwachukua dakika ya 25 Azam FC kuweza kupata bao la uongozi, likifungwa na Zayed alipokea pasi safi ya Shaaban na kuwatoka mabeki wa Ndanda kabla ya kupiga shuti zuri nje kidogo ya eneo la 18 lililotinga wavuni.
    Dakika tano baadaye Azam FC ilinufaika kwa mpira wa adhabu ndogo, baada ya winga Enock Atta kuitumia vema na kufunga bao la pili kwa mpira wa moja kwa moja uliomshinda kipa wa Ndanda, Jeremiah Kisubi.
    Ndanda ilirejea mchezoni na kujipatia bao lake pekee lililofungwa na Nassor Kapama, kwa mkwaju wa moja kwa moja wa adhabu ndogo uliomshinda kipa wa Azam FC, Razak Abalora na kufanya mpira huo uende mapumziko kwa wenyeji hao kuogoza 2-1.
    Azam FC ilihitimisha ushindi wake kipindi cha pili baada ya Shaaban kuipatia bao la tatu akifunga kiustadi akiunganisha pasi safi ya juu ya winga Idd Kipagwile, ambaye naye alikuwa kwenye kiwango kizuri.
    Katika mchezo huo, Azam FC ilimkosa Kocha wake Mkuu, Aristica Cioaba, ambaye alikuwa jukwaani baada ya kufungiwa na Bodi ya Ligi (TPLB) wakidai alionyesha ishara mbaya kwa mashabiki kwenye mchezo uliopita dhidi ya Yanga.
    Huu ni mwendelezo wa Bodi hiyo kuendelea kumsakama kocha huyo bila ushahidi dhahiri, ambapo hii ni mara ya pili inamfungia, kifungo cha awali wakimuhusisha ametoa lugha chafu kwa waamuzi wakati wa mchezo wa Azam FC dhidi ya Ruvu Shooting.
    Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kitaendelea kuwepo kambini kujiandaa na mchezo ujao dhidi ya Simba utakaofanyika Uwanja wa Taifa Jumatano ijayo saa 10.00 jioni, ambapo kesho Jumapili itaanza programu kujiandaa na mechi hiyo.
    Kikosi cha Azam FC leo: Razak Abalora, Daniel Amoah, Bruce Kangwa/David Mwantika dk 58, Yakubu Mohammed, Agrey Moris, Frank Domayo, Enock Atta, Salmin Hoza, Yahya Zayd/Ramadhan Singano dk 74, Shaaban Idd/Paul Peter dk 68, Idd Kipagwile.
    Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Yanga imeshinda 2-0 dhidi ya wenyeji, Lipuli mabao ya Papy Kabamba Tshishimbi na Pius Buswita, Singida United imeichapa 3-2 Mwadui FC, Tanzania Prisons imeshinda 2-0 dhidi ya Njombe Mji FC na Maji Maji FC imelala 2-1 mbele ya Mbeya City Uwanja wa Sokoine, Mbeya.   
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC YARUDI NAFASI YA PILI LIGI KUU BAADA YA KUIPIGA NDANDA 3-1 CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top