• HABARI MPYA

  Friday, January 13, 2017

  NI AZAM, AU SIMBA BINGWA MAPINDUZI LEO?

  Na Mwandishi Wetu, ZANZIBAR
  VIGOGO wa Tanzania Bara, Simba na Azam wanakutana katika fainali ya Kombe la Mapinduzi usiku wa leo Uwanja wa Amaan, visiwani Zanzibar.
  Mchezo huo unaotarajiwa unatarajiwa kuanza Saa 2:15 usiku wa leo, utakuwa ni wa pili kuzikutanisha timu hizo katika fainali ya michuano hiyo.
  Awali zilikutana katika fainali ya mwaka 2012 na Azam FC ikaibuka na ushindi wa mabao 2-1 na kutwaa taji lake la kwanza kati ya mawili ya Kombe la Mapinduzi, linguine likija mwaka 2013 baada ya kuifunga Tusker katika fainali.
  Simba ndiyo mabingwa mara nyingi wa taji hilo, mara tatu baada ya awali kulitwaa katika miaka ya 2008 ikiifunga Mtibwa Sugar katika fainali, 2011 ikiwafunga mahasimu, Yanga na 2015 wakiwafunga Mtibwa Sugar. 
  Azam mara zote ilizoingia fainali ilitwaa taji hilo, wakati Simba mwaka 2012 na 2014 ilicheza mechi ya mwisho kwa machungu baada ya kufungwa na kukosa na Kombe hilo.
  Kuelekea mchezo wa leo, kila timu iko vizuri baada ya rekodi nzuri katika mechi zilizopita, Simba wakiwatoa wapinzani wa jadi, Yanga kwa penalti 4-2 baada ya sare ya 0-0 kwenye Nusu Fainali na Azam wakiitoa Taifa Jang’ombe kwa bao 1-0.
  Timu zote ziliongoza makundi yao, Simba A lilikuwa na timu tano kwa pointi zake 10 na Azam B lililokuwa na timu nne kwa pointi zake saba.  
  Na timu zote zinakutana baada ya kila timu kuboresha kikosi chake kwa usajili mdogo wa dirisha dogo Desemba mwaka jana, upande wa Simba ikiingiza wachezaji watatu wapy, Waghana kipa Daniel Agyei, kiungo James Kotei na mshambuliaji mzawa, Pastory Athanas kutoka Stand United.
  Azam iliwasajili Waghana Yakubu Mohammed, Enock Atta Agyei, Yahya Mohammed na Samuel Afful na Mcameroon Stephan Mpondo pamoja na mzawa, Joseph Mahundi.
  Na wachezaji wote hao wapya wametokea kuwa muhimu kwenye timu na wanapewa nafasi kubwa ya kutumika na leo pia.
  Katika mechi zote za awali za Mapinduzi, Azam ilikuwa chini ya makocha wa Muda, Iddi Nassor Cheche na Iddi Abubakar Mwinchumu baada ya kuwafukuza makocha wake Waspaniola chini ya Zeben Hernandez Rodriguez, lakini baada ya kuingia fainali ikamtangaza kocha mpya, Mromania Aristica Cioaba. 
  Simba SC yenyewe itaendelea kuwa chini ya kocha wake Mcameroon, Joseph Marius Omog anayesaidiwa na Mganda, Jackson Mayanja.
  Vikosi vinatarajiwa kuwa; Simba; ⁠⁠Daniel Agyei, Janvier Bokungu, Mohammed Hussein 'Tshabalala', Abdi Banda, Method Mwanjali, Jonas Mkude, Shiza Kichuya, James Kotei, Juma Luizio, Laudit Mavugo na Muzamil Yassin. 
  Azam FC; Aishi Manula, Shomary Kapombe, Gardiel Michael, Aggrey Morris, Yakubu Mohammed, Stephan Mpondo, Joseph Mahundi, Frank Domayo, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, John Bocco ‘Adebayor’ na Yahya Mohammed.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NI AZAM, AU SIMBA BINGWA MAPINDUZI LEO? Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top