• HABARI MPYA

    Sunday, March 27, 2016

    MAAMUZI MABOVU ZAIDI KUWAHI KUTOKEA NCHINI

    WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michuano ya Afrika, Azam na Yanga wote watacheza mechi tatu za mashindano ya nyumbani, kabla ya kucheza mechi zao za kwanza Raundi za Pili za michuano hiyo.
    Kila timu itacheza mechi moja ya Kombe la Shirikisho Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation Machi 31 na Aprili 3 na 6 timu hizo zitacheza mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Hizo ni mechi za viporo ambazo ziliahirishwa wakati timu hizo zikiwa kwenye mechi zake za awali za michuano ya Afrika.
    Yanga walianzia Raundi ya Awali wakaitoa Cercle de Joachim ya Maurtius kwa jumla ya mabao 3-0, wakishinda 1-0 ugenini na 2-0 nyumbani.

    Katika Raundi ya kwanza wakaitoa APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2 wakishinda 2-1 ugenini na kabla ya kutoa sare ya 1-1 nyumbani.
    Azam FC wao walianzia Raundi ya kwanza na wakaitoa Bidvest Wits ya Afrika Kusini kwa ushindi wa jumla wa 7-3, wakishinda 3-0 ugenini na 4-3 nyumbani.
    Yanga sasa itamenyana na Al Ahly ya Misri Aprili 9, wakati Azam FC itamenyana na Esperance ya Tunisia, Aprili 10, mechi zote zikichezwa Dar es Salaam. Mechi za marudiano zitachezwa kati ya Aprili 18 na 20.
    Al Ahly (National) na Esperance zote ni timu bora na miaka yote wamekuwa washindani wa mataji ya Afrika – hii inamaanisha timu zetu sasa zinaingia kwenye mtihani mgumu na zinahitaji maandalizi ya kina.
    Tayari miongoni mwetu tumekwishahukumu kwamba mwisho wa safari za Azam na Yanga kwenye michuano ya Afrika umewadia, tu kwa sababu tunajua ubora na umakini wa hali ya juu wa Ahly na Esperance katika michuano hiyo.
    Na hii pekee ni sababu tosha kwamba, Azam na Yanga zinahitaji maandalizi mazuri. Kumekuwa na malalamiko ya baadhi ya timu katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara juu ya kuahirishwa kwa mechi za Azam na Yanga kwa ajili ya mechi za Afrika, Simba SC wakiongoza kelele hizo.
    Simba wanataka Azam na Yanga waendelee na ligi huku wakicheza michuano ya Afrika pia – si vibaya, lakini tukiweka mbele maslahi ya taifa, ipo haja ya kulitazama mara mbili suala hilo.
    Mshambuliaji tegemeo la mabao wa Yanga, Amissi Tambwe ameshindwa kucheza vizuri mechi zote dhidi ya APR kwa sababu aliumia katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya African Sports siku tatu kabla ya mchezo wa kwanza na APR mjini Kigali.
    Ni kweli Yanga na Azam zote zimesajili zaidi ya wachezaji 25, lakini lazima tukubali kwamba kati ya hao kuna wachezaji muhimu, ndiyo maana hata Barcelona pamoja na kuwa na wigo mpana wa wachezaji kuanzia wa kikosi cha kwanza, akiba na hata katika akademi yake, lakini bado utaona kuanzia mashindano ya nyumbani hadi Ulaya wanacheza wale wale akina Lionel Messi, Neymar, Luis Suarez na wenzao.
    Usipomuona mmoja kati ya wachezaji unaowajua wa kikosi cha kwanza cha Barca, basi jua atakuwa anaumwa au anatumikia adhabu. Huo ndiyo ukweli. Wakati Yanga na Azam wanatarajiwa kucheza na wapinzani wao wa Kaskazini mwa Afrika Aprili 9 na 10 Dar es Salaam, kabla ya hapo watakuwa na mechi mbili za mashindano ya nyumbani, Kombe la TFF na Ligi Kuu.
    Wazi huku ni kuzitengenezea mazingira mabaya timu hizo kuelekea kwenye mechi hizo ngumu za michuano ya Afrika.
    Ipo haja Bodi ya Ligi na TFF pamoja na malalamiko yaliyopo wakatumia hekima ba busara wawezavyo ili kuziwezesha Azam na Yanga kupata fursa nzuri ya maandalizi kabla ya mechi zao na Ahly na Esperance. 
    Wayapime malalamiko ya Simba na wapime uzito wa majukumu ya Yanga na Azam na kuangalia umuhimu wa kila jambo.
    Tunacheza Ligi na Kombe la TFF ili mwisho wa siku kuwapata mabingwa, ambao watatuwakilisha kwenye michuano ya Afrika.
    Na tumekuwa mstari wa mbele kulalamikia matokeo mabaya ya timu zetu kwenye michuano ya Afrika, huku pia tukilaumu maandalizi ya zimamoto.
    Simba SC walifika fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993, lakini ukitazama safari yao kabla ya kufika hapo, utaona walipewa nafasi ya kwenda kuweka kambi Nice, Ufaransa.
    Simba hao hao waliwatoa Zamalek ya Misri mwaka 2003 katika Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini ukitazama safari yao utaona walipewa fursa ya kwenda kuweka kambi Oman.
    Lakini Simba hao hao, leo wapo mstari wa mbele kulalamika Azam na Yanga kuahirishiwa mechi zao za Ligi ili wapate fursa nzuri ya maandalizi ya michuano ya Afrika.
    Sitaki kusema Simba ni wabinafasi, naweza kuhisi ni kiu ya ubingwa ambao wameukosa kwa miaka mitano inawafanya wasahau hata umuhimu wa mambo yenye faida kwa taifa zima.
    Kwa kuwa Simba wanaongoza ligi, wanataka ichezwe, iendelee kuchezwa haraka iishe watwae ubingwa – lakini wanasahu wakiwa mabingwa na wao watapitia mitihani ambayo Azam na Yanga wanapitia sasa.
    Nadhani tuweke kando ubinafsi na tuzitazame Azam na Yanga katika sura ya kitaifa zaidi na faida zake iwapo zitafanya vizuri.
    Simba na TFF lazima wajue kwamba iwapo Azam na Yanga watafanikiwa kuingia hatua ya makundi ya michuano ya Afrika, upo uwezekano tukaongezewa nafasi za kuingiza timu kwenye michuano hiyo kutoka mbili za sasa. 
    Lakini pamoja na ukweli huo, Mtendaji wa Bodi ya Ligi, Boniphace Wambura jana amekaririwa akisema kwamba Yanga na Azam zimeandika barua za kuomba kuahirishiwa baadhi ya mechi za wiki ya mechi zao za michuano ya Afrika, lakini wamewakatalia.
    Hili ni taifa ambalo linapambana kujiinua kisoka, lakini inasikitisha viongozi wake wanashindwa kuwa na mipango ya kufanikisha hilo.
    Kama kuna makosa yalifanyika awali hadi Azam na Yanga leo wana mechi nyingi za viporo, hayawezi kufutika kwa kuzilazimisha timu hizo kucheza mechi nyingi ndani ya muda mfupi.
    Sana Azam na Yanga zilihitaji japo wiki nzima ya maandalizi tu kwa mechi dhidi ya timu hizo kali za Kaskazini mwa Afrika, lakini kuzilazimisha zicheze mechi tatu kwanza za mashindano ya nyumbani ni maamuzi mabovu zaidi kuwahi kutokea nchini kwenye masuala ya aina hiyo. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAAMUZI MABOVU ZAIDI KUWAHI KUTOKEA NCHINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top