• HABARI MPYA

  Jumatano, Machi 30, 2016

  MAYANJA 'AWANYOROSHA' VICHWA NGUMU SIMBA SC

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KIWANGO cha nidhamu ya wachezaji ndani ya klabu ya Simba sasa kinaridhisha, baada ya uongozi kuamua kuunga mkono juhudi za kocha Mganda, Jackson Mayanja (pichani kushoto) dhidi ya wachezaji ‘watukutu’.
  Mayanja alianza kupambana na beki Hassan Isihaka ambaye alithubutu kumuuliza kocha huyo Mganda maswali ya kifedhuli na uongozi ukamfungia kwa mwezi mmoja mchezaji huyo.
  Na wiki mbili zilizopita Mayanja alihamia kwa beki mwingine anayeweza kucheza kama kiungo pia, Abdi Banda ambaye alikaidi agizo la kuinuka kupasha misuli moto ili aingie kuchukua nafasi ya Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ mwanzoni mwa mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
  Baada ya mchezo, Banda alishauriwa kwenda kumuomba msamaha kocha Mayanja, lakini akakaidi tena na uongozi ukamuandikia barua ikimtaka kutoa maelezo juu ya utovu huo wa nidhamu.
  Wakati Banda amekwishawasilisha barua yake na matarajio ni naye kufungiwa, wachezaji wengine wa Simba sasa wameingiwa woga na kocha huyo.
  Woga huo umewafanya wawe watiifu mno kwa Mganda huyo – hali ambayo inatafsiriwa kama ni kurejea kwa nidhamu inayotakiwa kikosini.
  Inaaminika kwa muda mrefu wachezaji wengi wa Simba wamekuwa hawawaheshimu makocha kutokana na kutiwa kiburi na baadhi ya viongozi.
  Lakini kutokana na mambo kubadilika sasa Msimbazi na Mayanja kupewa mamlaka kamili ya kuwaongoza wachezaji, nidhamu inatarajiwa kurejea kwa asilimia 100.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MAYANJA 'AWANYOROSHA' VICHWA NGUMU SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top