• HABARI MPYA

  Jumanne, Machi 29, 2016

  NYOTA WA AHLY AITUPA NJE NIGERIA AFCON 2017

  BAO pekee la Ramadan Sobhi (pichani kulia) limeipa ushindi wa 1-0 Misri katika mchezo wa Kundi G kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika leo Uwanja wa Borg El Arab mjini Cairo.
  Kiungo huyo mshambuliaji wa Al Ahly, alifunga bao hilo dakika ya 66 na sasa na sasa Mafarao wanazidi kupaa kileleni mwa kundi hilo wakifikisha pointi saba baada ya kucheza mechi tatu.
  Nigeria inayobaki na pointi mbili sasa inatupwa nje ya mbio za AFCON ya mwakani, kwani hata wakiifunga Tanzania katika mchezo wake wa mwisho Septemba 2 watafikisha pointi tano katika kundi ambalo inafuzu timu moja tu. Misri itakwenda Dar es Salaam kutafuta sare kwa Tanzania ili kujihakikishia kufuzu.
  Tanzania inashika mkia katika Kundi G, lakini ina michezo miwili mkononi dhidi ya zote, Misri nyumbani na Nigeria ugenini, ambazo ikishinda zote itamaliza pointi sawa na Mafarao na timu ya kufuzu itatazamwa kwa wastani wa mabao.   
  Mjini Kigali, kiungo wa Azam FC, Jean Baptiste Mugiraneza amefunga bao moja, Rwanda ikishinda 5-0 dhidi ya Mauritius katika mchezo wa Kundi H. Mabao mengine ya Amavubi yamefungwa na N D Savior, Ernest Sugira mawili na F Omborenga.
  Mjini Bujumbura, kiungo wa zamani wa Simba ya Tanzania, Pierre Kwizera amefunga bao moja, Burundi wakiilaza 3-1 Namibia katika mchezo wa Kundi K.
  Mabao mengine ya Burundi yamefungwa na Abdul Razak Fiston wakati la Namibia waliotangulia limefungwa na D Hotto.
  Angola imefungwa nyumbani 2-0 na DRC, wakati Afrika Kusini imelazimishwa sare ya 0-0 na Cameroon Uwanja wa Moses Mabhida sawa na Gambia ambao pia wametoka 0-0 na Mauritania.
  Liberia imeichapa 5-0 Djibouti, Lesotho imeifunga 2-1 Shelisheli nyumbani, wakati Uganda imelazimishwa sare ya 0-0 na Burkina Faso mjini Kampala, sawa na Togo iliyotoa 0-0 na Tunisia nyumbani, huku Ethiopia ikilazimishwa sare ya 3-3 na Algeria nyumbani na Senegal ikishinda 2-1 ugenini dhidi ya Niger sawa na Guinea iliyoifunga 2-1 Malawi mjini Blantyre.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: NYOTA WA AHLY AITUPA NJE NIGERIA AFCON 2017 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top