• HABARI MPYA

  Alhamisi, Machi 24, 2016

  HANS POPPE: AZAM WATAKULA JEURI YAO

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema Azam FC inalazimika kuvuna matunda ya ukaidi wao kwa kwenda kucheza ‘bonanza’ Zambia na kuacha Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ikiendelea.
  “Hatukatai Azam na Yanga kupewa muda wa maandalizi wa mashindano yao ya Afrika, lakini huko nyuma walikwishakosea kwa kwenda kucheza bonanza na kuacha ligi,”.
  “Matokeo yake sasa wanazidi kulundikiwa mechi za viporo na kupoteza ladha ya ligi, kama wasingekwenda Zambia, wasingekuwa na viporo vingi, ila kwa kuwa walikaidi mawazo ya timu nyingine, sasa wacheze Ligi,”amesema Hans Poppe.  
  Zacharia Hans Poppe (kushoto) amesema Azam FC watakula jeuri yao

  Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), amesema kwamba Azam walijitakia wenyewe kuacha ligi na kwenda kucheza bonanza na sasa umefika wakati wanahitaji huruma ya dhati, lakini hawawezi kuipata kwa sababu walikwishakosea huko nyuma.
  Hans Poppe ameiomba TFF, Bodi ya Ligi na wahusika wote kuchukulia makosa yaliyotokea kama fundisho na siku nyingine wasije kurudia.
  Januari mwaka huu, Azam walikwenda Zambia kushiriki michuano maalum ya kirafiki ambako waliibuka mabingwa, igawa Ligi Kuu iliendelea na wao mechi zao zikapangiwa tarehe nyingine.
  Na sasa Azam FC ipo kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na Aprili 10 watamenyana na Esperance ya Tunisa Dar es Salaam katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Pili.
  Wakiwa wanahitaji muda mzuri wa maandalizi, Azam FC watalazimika kucheza mechi za Kombe la TFF na za Ligi mbili katika wiki ambayo watacheza na Esperance.
  Mtihani kama huo unawakabili pia mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Yanga ambao watamenyana na Al Ahly ya Misri Aprili 9 katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wakitoka kucheza mechi mbili za viporo za Ligi Kuu na moja ya Kombe la TFF.
  Simba SC ndiyo inaongoza Ligi Kuu kwa sasa ikiwa na pointi 57, ikifuatiwa na Azam na Yanga zenye 50 kila moja, lakini Wekundu wa Msimbazi wana mechi tatu zaidi ya wapinzani wao hao kwenye mbio za ubingwa (24-21).
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: HANS POPPE: AZAM WATAKULA JEURI YAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top