• HABARI MPYA

  Jumamosi, Machi 26, 2016

  NIGERIA SARE NA MISRI, IVORY COAST YAAMKA

  TIMU ya taifa ya Nigeria imelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Misri katika mchezo wa Kundi G kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika leo mjini Kaduna.
  Oghenekaro Etebo alianza kuifungia Nigeria dakika ya 60, akimalizia mpira uliorudi baada ya kufonga mwamba kufuatia shuti la Kelechi Iheanacho.
  Hata hivyo, Mohammed Salah akaisawazishia Misri dakika ya mwisho na kuwazima mashabiki wa nyumbani.
  Sare hiyo inaifanya Misri ifikishe pointi saba na kuendelea kuongoza kundi hilo, ikifuatiwa na Nigeria yenye pointi tano sasa, wakati Tanzania iliyoifunga Chad mjini D'jamena Jumatano ni ya tatu kwa pointi zake nne.
  Nigeria imelazimishwa sare ya 1-1 nyumbani na Misri leo
  Nigeria na Misri zitarudiana mjini Alexandria Jumanne, wakati Tanzania na Chad zitarudiana Dar es Salaam Jumatatu.
  Ikumbukwe mshindi wa kundi tu ndiye atafuzu kwa fainali za mwakani za AFCON nchini Gabon.
  Mabingwa watetezi nao, Ivory Coast wamepata ushindi wa kwanza Kundi I baada ya kuilaza 1-0 Sudan Uwanja wa Felix Houphouet-Boigny mjini Abidjan, bao pekee la Gervinho dakika ya 34.
  Tembo wa Ivory Coast waliotoa sare ya bila kufungana katika mechi zao mbili za mwanzo dhidi ya Gabon na Sierra Leone, sasa wanafikisha pointi tano na kupanda nafasi ya pili nyuma ya Gabon wenye pointi saba, wakati Sudan ni ya tatu kwa pointi zake tatu na Sierra Leone yenye pointi moja inashika mkia.
  Mechi nyingine za leo, Algeria imeifunga 7-1 Ethiopia Uwanja wa Mustapha Tchaker, Mali imeifunga 1-0 Equatorial Guinea Uwanja wa Machi 26, Guinea imetoa sare ya 0-0 Malawi Uwanja wa Septemba 28, Tunisia imeifunga 1-0 Togo Uwanja wa Mustapha Ben Jannet, Mauritania imeifunga 2-1 Gambia Uwanja wa Nouakchott na Swaziland imelazimishwa sare ya 1-1 na  Zimbabwe.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: NIGERIA SARE NA MISRI, IVORY COAST YAAMKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top