• HABARI MPYA

  Jumatano, Machi 23, 2016

  NGASSA AANZA KUJIFUA GYM

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  MCHEZAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mrisho Khalfan Ngassa ameanza mazoezi mepesi ya gym baada ya kupata nafuu kufuatia upasuaji wa mguu mwezi uliopita.
  "Nimeanza mazoezi mepesi jana, nafanya gym tu. Lakini namshukuru Mungu ninaendelea vizuri,"amesema Ngassa akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE kutoka Bethlehem, Afrika Kusini jana.
  Mshambuliaji huyo wa Free State Stars, Ngassa aliumia mapema mwaka huu katika mchezo wa Ligi Kuu ya ABSA Afrika Kusini na baada ya vipimo ikaonekana anahitaji kufanyiwa upasuaji.
  Mrisho Ngassa akijifua kwenye gym jana baada ya kupata nafuu ya maumivu yake kufuatia kufanyiwa upasuaji mdogo mwezi uliopita
  Ngassa anapambana ili arejee uwanjani mwezi ujao kwa nguvu mpya
  Mrisho Ngassa ameitakia kila la heri timu yake ya taifa, Taifa Stars ambayo leo inamenyana na Chad
  Ngassa ameanza mazoezi ya gym kwa nguvu tangu jana jioni mjini Bethlehem, Afrika Kusini

  Ngassa ambaye maumivu hayo yamemsababisha aukose mchezo kati ya timu yake ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars na Chad leo kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika amesema kwamba kama mambo yataendelea hivyo anatarajiwa katikati ya mwezi ujao ataanza kucheza.
  "Kwa ninavyoona sasa maendeleo yangu, kama hali itaendelea hivi, basi nadhani mwezi ujao katikati hivi naweza kurudi uwanjani,"amesema.
  Pamoja na hayo, Ngassa ameitakia kila la heri Taifa Stars katika mchezo wake wa leo dhidi ya Chad mjini D'jamena. 
  "Naitakia kila la heri timu yangu ya taifa, nawaamini wanajeshi wenzangu, na ninaamini jioni watatufanya Watanzania wote tufurahie ushindi, Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Taifa Stars,"amesema fundi wa mpira, Ngassa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: NGASSA AANZA KUJIFUA GYM Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top