• HABARI MPYA

    Wednesday, March 23, 2016

    NYUMA YA MAFANIKIO YA SIMBA 1993, 2003…YANGA NA AZAM JE?

    WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michuano ya Afrika, Azam na Yanga wote wamefanikiwa kuingia Raundi za Pili za michuano hiyo baada ya kuwatoa wapinzani wao mwishoni mwa wiki.
    Yanga walianza kuwatoa APR ya Rwanda katika Ligi ya Mabingwa Afrika Jumamosi baada ya sare ya 1-1 wakitoka kushinda 2-1 ugenini mjini Kigali wiki iliyotangulia na Azam FC wakafuatia Jumapili kwa kuwatoa Bidvest Wits ya Afrika Kusini baada ya ushindi wa mabao 4-3 wakitoka kushinda 3-0 ugenini mjini Johannesburg.

    Maana yake, Yanga imesonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 3-2 na sasa itamenyana na Al Ahly ya Misri mwezi ujao, wakati Azam FC imefuzu kwa ushindi wa jumla wa 7-3 na sasa itamenyana na Esperance ya Tunisia, pia mwezi ujao.
    Mechi za kwanza zinatarajiwa kuchezwa kati ya Aprili 8 na 10, wakati marudiano yatakuwa kati ya Aprili 18 na 20 na timu zote za Tanzania zitaanzia nyumbani.
    Al Ahly (National) na Esperance zote ni timu bora na miaka yote wamekuwa washindani wa mataji ya Afrika – hii inamaanisha timu zetu sasa zinaingia kwenye mtihani mgumu na zinahitaji maandalizi ya kina.
    Tayari miongoni mwetu tumekwishahukumu kwamba mwisho wa safari za Azam na Yanga kwenye michuano ya Afrika umewadia, tu kwa sababu tunajua ubora na umakini wa hali ya juu wa Ahly na Esperance katika michuano hiyo.
    Na hii pekee ni sababu tosha kwamba, Azam na Yanga zinahitaji maandalizi mazuri. Kumekuwa na malalamiko ya baadhi ya timu katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara juu ya kuahirishwa kwa mechi za Azam na Yanga kwa ajili ya mechi za Afrika, Simba SC wakiongoza kelele hizo.
    Simba wanataka Azam na Yanga waendelee na ligi huku wakicheza michuano ya Afrika pia – si vibaya, lakini tukiweka mbele maslahi ya taufa, ipo haja ya kulitazama mara mbili suala hilo.
    Mshambuliaji tegemeo la mabao wa Yanga, Amissi Tambwe ameshindwa kucheza vizuri mechi zote dhidi ya APR kwa sababu aliumia katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya African Sports siku tatu kabla ya mchezo wa kwanza na APR mjini Kigali.
    Ni kweli Yanga na Azam zote zimesajili zaidi ya wachezaji 25, lakini lazima tukubali kwamba kati ya hao kuna wachezaji muhimu, ndiyo maana hata Barcelona pamoja na kuwa na wigo mpana wa wachezaji kuanzia wa kikosi cha kwanza, akiba na hata katika akademi yake, lakini bado utaona kuanzia mashindano ya nyumbani hadi Ulaya wanacheza wale wale akina Lionel Messi, Neymar, Luis Suarez na wenzao.
    Usipomuona mmoja kati ya wachezaji unaowajua wa kikosi cha kwanza cha Barca, basi jua atakuwa anaumwa au anatumikia adhabu. Huo ndiyo ukweli. Wakati Yanga na Azam wanatarajiwa kucheza na wapinzani wao wa Kaskazini mwa Afrika Aprili 9 na 10 Dar es Salaam, kabla ya hapo watakuwa na mechi mbili za mashindano ya nyumbani, Kombe la TFF na Ligi Kuu.
    Wazi huku ni kuzitengenezea mazingira mabaya timu hizo kuelekea kwenye mechi hizo ngumu za michuano ya Afrika.
    Ipo haja Bodi ya Ligi na TFF pamoja na malalamiko yaliyopo wakatumia hekima ba busara wawezavyo ili kuziwezesha Azam na Yanga kupata fursa nzuri ya maandalizi kabla ya mechi zao na Ahly na Esperance. 
    Wayapime malalamiko ya Simba na wapime uzito wa majukumu ya Yanga na Azam na kuangalia umuhimu wa kila jambo.
    Tunacheza Ligi na Kombe la TFF ili mwisho wa siku kuwapata mabingwa, ambao watatuwakilisha kwenye michuano ya Afrika.
    Na tumekuwa mstari wa mbele kulalamikia matokeo mabaya ya timu zetu kwenye michuano ya Afrika, huku pia tukilaumu maandalizi ya zimamoto.
    Simba SC walifika fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993, lakini ukitazama safari yao kabla ya kufika hapo, utaona walipewa nafasi ya kwenda kuweka kambi Nice, Ufaransa.
    Simba hao hao waliwatoa Zamalek ya Misri mwaka 2003 katika Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini ukitazama safari yao utaona walipewa fursa ya kwenda kuweka Oman.
    Lakini Simba hao hao, leo wapo mstari wa mbele kulalamika Azam na Yanga kuahirishiwa mechi zao za Ligi ili wapate fursa nzuri ya maandalizi ya michuano ya Afrika.
    Sitaki kusema Simba ni wabinafasi, naweza kuhisi ni kiu ya ubingwa ambao wameukosa kwa miaka mitano inawafanya wasahau hata umuhimu wa mambo yenye faida kwa taifa zima.
    Kwa kuwa Simba wanaongoza ligi, wanataka ichezwe, iendelee kuchezwa haraka iishe watwae ubingwa – lakini wanasahu wakiwa mabingwa na wao watapitia mitihani ambayo Azam na Yanga wanapitia sasa.
    Nadhani tuweke kando ubinafsi na tuzitazame Azam na Yanga katika sura ya kitaifa zaidi na faida zake iwapo zitafanya vizuri.
    Simba na TFF lazima wajue kwamba iwapo Azam na Yanga watafanikiwa kuingia hatua ya makundi ya michuano ya Afrika, upo uwezekano tukaongezewa nafasi za kuingiza timu kwenye michuano hiyo kutoka mbili za sasa. 
    Je, itakuwa faida kubwa kiasi gani? Basi tutumie hekima na busara katika hili, lakini ukweli ni kwamba Azam na Yanga zinahitaji nafasi ya kutosha ya maandalizi kabla ya mechi na Ahly na Esperance. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NYUMA YA MAFANIKIO YA SIMBA 1993, 2003…YANGA NA AZAM JE? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top