• HABARI MPYA

  Ijumaa, Machi 25, 2016

  AZAM NOMA, YAIPIGA 'WIKI' RANGERS CHAMAZI

  KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, asubuhi ya leo imeichapa Friends Rangers mabao 7-1 katika mchezo wa kirafiki wa mazoezi uliofanyika katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, jijini Dar es Salaam.
  Mchezo huo ulikuwa ni maalumu kwa ajili ya benchi la ufundi kuwaangalia na kuwapima wachezaji ambao hawajapata muda mwingi wa kucheza msimu huu pamoja na wale wasiokuwepo katika majukumu ya timu zao za Taifa.
  Benchi la ufundi pia lilitumia fursa hiyo kuwajaribu wachezaji wanne wa Azam FC Academy, beki Joshua John, viungo Ferej Khamis ‘Ozil’, Rajabu Odas na mshambuliaji Shaaban Idd, ambao walifanikiwa kuonyesha viwango vizuri.  
  Hadi kipindi cha kwanza cha mchezo huo kinamalizika, Azam FC ilikuwa mbele kwa mabao 4-0, yaliyofungwa na Ramadhan Singano ‘Messi’ dakika ya pili kwa mpira wa moja kwa moja wa adhabu ndogo, kabla ya kiungo Michael Bolou kuongeza la pili dakika tatu baadaye kwa shuti kali nje ya eneo la 18.
  Kiungo wa Azam FC, Frank Domayo akitafuta maarifa ya kupaua katikati ya wachezaji wa Friends Rangers
  Kiungo wa Azam FC, Salum Abubakr 'Sure Boy' akiwatoka wachezaji wa Friends Rangers

  Mshambuliaji Didier Kavumbagu naye akapiga la tatu dakika ya 37 baada ya kupokea pasi safi ya Messi, dakika sita baadaye kabla ya mpira kwenda mapumziko kiungo Mudathir Yahya aliongeza la nne.
  Jumla ya mabao matatu yaliongezeka kipindi cha pili yakifungwa na wachezaji walioingia kipindi hicho, kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ (dk52), winga Khamis Mcha ‘Vialli’ (dk46) na kinda Shaaban Idd (dk86), huku Allan Wanga akikosa mkwaju wa penalti uliopatikana baada ya Mcha kuangushwa na kipa wa Friends inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL).
  Friends Rangers yenyewe ilijipatia bao lao la kufutia machozi dakika ya 73 kupitia kwa nyota wao Cosmas Lewis kwa mkwaju wa penalti baada ya Aggrey Morris kumfanyia madhambi mchezaji mmoja wa Friends ndani ya eneo la 18.
  Katika jambo la kufurahisha zaidi, Rangers ilimtumia winga wa Azam FC, Joseph Kimwaga, katika mchezo huo aliyepelekwa kwa mkopo kwenye timu ya Simba, huku pia kikosini kwao ikiwa na wachezaji wengine waliowahi kuwika na kupitia ndani ya Academy ya Azam FC kama vile nahodha wa zamani wa kikosi hicho, Abdul Mgaya.
  Azam FC iliyoanza mazoezi jana mara baada ya mapumziko ya siku tatu, katika mchezo huo ilipata pigo dakika ya 36 baada ya kuumia goti kwa beki wake kushoto Gadiel Michael na nafasi yake ikachukuliwa na Wazir Salum ‘Waza’.
  Mara baada ya mchezo huo, Kocha Msaidizi wa Azam FC, Mario Marinica alifurahishwa na viwango vya wachezaji waliocheza mchezo huo akisema kuwa wananafasi ya kufanya vema zaidi uwanjani katika mechi zinazokuja kama wakiendelea kucheza kwa namna hiyo.
  Jumla ya wachezaji wa nane wa Azam FC inayodhaminiwa na Benki bora kabisa nchini ya NMB, wameukosa mchezo huo kutokana na kuwa kwenye majukumu ya timu zao za Taifa, saba wakiwa Tanzania ‘Taifa Stars’ na Jean Mugiraneza akiwa Rwanda ‘Amavubi’.
  Kikosi cha Azam FC leo kilikuwa; Mwadini Ally/Ivo Mapunda dk46, Ramadhan Singano/Rajab Odas dk61, Gardiel Michael/Waziri Salum dk36, Serge Wawa/Aggrey Morris dk46, Racine Diouf/Abdallah Kheri dk46, Said Mourad/Joshua John dk61, Frank Domayo/Ferej Khamis dk61, Michael Bolou/Salum Abubakar dk46, Mudathir Yahya/Shaaban Idd dk61, Allan Wanga na Didier Kavumbagu/Khamis Mcha dk46. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AZAM NOMA, YAIPIGA 'WIKI' RANGERS CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top