• HABARI MPYA

  Alhamisi, Machi 24, 2016

  YONDAN AKIMBIZWA HOSPITALI D’JAMENA

  Na Prince Akbar, ADDIS ABABA
  BEKI wa kati wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Kevin Yondan yuko kwenye hatihati ya kucheza mchezo wa marudiano dhidi ya Chad Jumatatu.
  Hiyo inafuatia beki huyo kukimbizwa hospitali baada ya mchezo wa kwanza na Chad jana Taifa Stars ikishinda 1-0 Uwanja wa Omnisports Idriss Mahamat Ouya mjini D’jamena.
  Katika mchezo huo wa Kundi G kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika, bao pekee la Taifa Stars lilifungwa na Nahodha, Mbwana Samatta anayechezea KRC Genk ya Ubelgiji dakika ya 30 akimalizia krosi ya Farid Mussa.
  Kevin Yondan (kushoto) na Mwinyi Kazimoto kabla ya mchezo wa jana mjini D'jamena

  Na baada ya mchezo huo tu, Yondan alipofika hotelini hali yake ilibadilika na kulalamika anasikia maumivu ya misuli, mbavu na mgongo.
  Hali hiyo ililazimu akimbizwe hospitali usiku ambako alitibiwa na kurejea hoteli ya kifahari zaidi mjini D’jamena, Ledger Plazza ambako Taifa Stars walifikia.
  “Ilionekana hali ya hewa ya joto kali ilichangia kuwa vile, tutaendelea kusikilizia hali yake tutakapofika nyumbani,”amesema Msemaji wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Baraka Kizuguto leo mjini D’jamena. 
  Kizuguto amesema kwa sasa Yondan, au Cotton Juice kwa jina la utani yupo katika uangalizi mzuri wa Daktari wa timu.
  Vikosi vyote, Chad na Tanzania vipo njiani kuelekea Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo wa marudiano Jumatatu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YONDAN AKIMBIZWA HOSPITALI D’JAMENA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top