• HABARI MPYA

  Jumatatu, Machi 21, 2016

  TWANGA PEPETA, DOUBLE M PLUS BADO TUNAWADAI

  Wakati mwingine huwa inafika wakati unajiuliza hivi baadhi ya bendi zetu zimelogwa? Hazijui wajibu wao? Hazijui nini wateja wanataka? Hawaelewi maana ya maonyesho maalum?
  Hivi bendi zetu zimewahi kujiuliza iwapo wateja wao wanataka muziki wa dansi au disco? Wanataka hotuba jukwaani au muziki wa dansi? Wanataka wasanii wanaoshambulia jukwaa au waliosimama kama wanaosubiri kukaguliwa gwaride?
  Hizo ni changamoto zisizokauka kwa baadhi ya bendi zetu ambazo zimevaa miwani ya mbao na ‘headphones’ za chuma – hazioni wala hazisikii ushauri wowote.

  Turejee kwenye maonyesho mawili makubwa yaliyofanyika wikiendi iliyopita (Ijumaa na Jumamosi) ndani ya ukumbi wa Mango Garden Kinondoni ambayo ama kwa hakika yaliteka hisia za mashabiki wa muziki wa dansi.
  Ni maonyesho yaliyofana sana na wakati mwingine inahitaji moyo wa chuma kuyakosoa, unaweza ukawa kama unawakatisha tamaa badala ya kuwajenga – mahudhurio yalinona (kulingana na soko la sasa), wasanii wakapendeza jukwaani kwa ‘pamba’ za maana, hali inayoonyesha kuwa pesa nyingi zilitumika kuandaa maonyesho hayo.
  Ijumaa walipiga Double M Plus wakitambulisha rasmi bendi, wasanii wapya na nyimbo mpya huku wenye nyumba Twanga Pepeta wakiibuka Jumamosi na onyesho lao lililoitwa “Twanga 18” lililodhamiria kusherehekea miaka 18 ya bendi sambamba na utambulisho wa wasanii wapya na nyimbo mpya.
  Nianze na onyesho la Twanga Pepeta ambalo binafsi naona lilibeba zaidi sura ya utambulisho wa wasanii wapya na nyimbo mpya kuliko kusherehekea miaka 18 ya bendi – hakukuwa na chochote kilichotoa picha ya kusherehekea umri huo mrefu wa bendi.
  Kwa maana nyingine ni kama vile Twanga walijinyima fursa ya kuwa na onyesho lingine kubwa ndani wiki kadhaa mbele – wangeweza kufanya onyesho lao la kutambulisha wasanii wapya na nyimbo mpya halafu miaka 18 ya bendi ikaja siku nyingine.
  Nilivutiwa sana na nyimbo mpya za Twanga Pepeta “Mtu Makini” na “Twanga Kwanza”, kwa sikio la kwanza tu nilitosheka kujiridhisha kuwa ni nyimbo bomba zinazoendana na soko la sasa. Rap mpya ya “Banjuka” kutoka kwa Ferguson nayo ilikuwa tamu sana.
  Onyesho lilikosa msisimko wa mashabiki kwenda kucheza na kutunza na  pengine hiyo ilichangiwa sana na uwepo wa matabaka ya tiketi za kawaida na za VIP, mazingira hayakuruhusu watu wa tiketi za kawaida (ambao ndiyo waliokuwa wengi zaidi) kwenda mbele kucheza au kutunza. Kwa kifupi jiografia ya Mango Garden haikidhi kuwa na matabaka ya tiketi.
  Je, Twanga Pepeta watamudu maisha bila wacheza show? Ni swali linalokuja baada ya wakati mwingine waimbaji wake kuonekana hawana umahiri sana wa kushambulia jukwaa, ni kama vile wameambiwa kazi hiyo ni ya madansa tu. Nadhani Twanga wanatakiwa kujenga mazoea ya kuwaficha wanenguaji wao kwenye baadhi ya nyimbo  itasaidia kuwafanya mashabiki wawe na kiu ya kuwaona madansa maana kuwaona katika kila wimbo inakinaisha, kuna wakati waimbaji wanapaswa kufanya kazi ya madansa. DENI HILO.

  Kwa upande wa Double M Plus, wao walipiga nyimbo nane mpya ambazo bado kabisa hazijafahamika miongoni mwa mashabiki wa dansi, lakini bado watu walionekana kuzifurahia, wakazisikiliza kwa makini. Kupiga nyimbo ambazo hazijulikani si jambo la masihara, unaweza kukuta nusu ya mashabiki wameondoka ukumbini.
  Nilichogundua ni kwamba Mwinjuma Muumin (mkurugenzi wa Double M Plus) bado anapendwa sana lakini watu hawataki aimbe vipande virefu – walimsifia sana kwenye nyimbo za “Ganda la Muwa”, Mapaungufu Yangu”, na “Siri ya Mgongo”  alizotupia vipande vifupi, lakini wakanong’ona chini kwa chini kulalamikia baadhi ya nyimbo alizoimba muda mrefu pale jukwaani. Tatizo la waimbaji  wa Double M Plus kutegemea zaidi madansa kwa kila nyimbo nalo lilikuwepo kama ilivyokuwa kwa Twanga Pepeta. DENI HILO, hapo ndipo mnapopigwa bao na ndugu zetu wa nchi jirani.
  Ukiachana na hayo, bendi hizo zilifanya vizuri katika maonyesho hayo na sasa deni kubwa wanalobakiwa nalo ni kuendeleza yale mazuri waliyoyafanya Ijumaa na Jumamosi na kuyahamishia  katika show zao za kila wiki na sio kusubiria maonyesho maalum pekee. Suala la usikivu mzuri wa vyombo nalo ni deni.
  Imarisheni uwajibikaji jukwaani, porojo zipunguzwe jukwaani, wasanii wanaohusika na wimbo ulioko hewani wawepo wote jukwaani na si kupiga domo na kwenye meza za wateja huku ukisubiri kipande chako ndo ukimbilie jukwaani. 
  Twanga Pepeta na Double M wameonyesha kuwa muziki wa dansi unaweza ukarejea kwenye hadhi yake, lakini hilo halitakuja kama hakutakuwa na ushirikiano mzuri baina ya wamiliki, wasanii, wadau na mashabiki kwa ujumla.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: TWANGA PEPETA, DOUBLE M PLUS BADO TUNAWADAI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top