• HABARI MPYA

  Jumapili, Machi 27, 2016

  CHAD WAIKACHA TAIFA STARS, WAJITOA 'KIMOJA' AFCON

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  TIMU ya taifa ya Chad imejitoa kwenye mechi za kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika mwakani na maana yake mchezo kati yao na Tanzania uliokuwa ufanyike kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam hautakuwepo.
  Katika barua yao kwenda Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Chad wamesema wamejitoa kwa sababu za kiuchumi kwamba hawana fedha za kuwawezesha kuendelea na mechi za Kundi G.
  Barua ya Chad kujitoa kufuzu AFCON
  Chad inajitoa baada ya kukamilisha mechi tatu za mzunguko wa kwanza, ikifungwa zote 2-0 na Nigeria ugenini, 5-1 na Misri nyumbani na 1-0 na Tanzania nyumbani Jumatano.
  Sasa Kundi G linabaki na timu tatu ambazo ni Tanzania, Nigeria na Misri.
  Chad hawajaja Tanzania na maana yake mechi ya kesho na Taifa Stars haitakuwepo, lakini bado CAF haijatoa taarifa yoyote juu ya hilo.
  Wenyeji Tanzania wamekuwa kambini hoteli ya Urban Rose, katikati ya Jiji la Dar es Salaam kwa maandalizi tangu warejee kutoka D’jamena, Chad Alfajiri ya Ijumaa baada ya mchezo wa kwanza walioshinda 1-0 Jumatano iliyopita. 
  Inaonekana kipigo cha Taifa Stars nyumbani kilichotokana na bao pekee la Mbwana Samata dakika ya 30 akimalizia krosi ya Farid Mussa ndicho kimewafanya Chad wajitoe wakiamini hawana nafasi tena na hapa sababu za kiuchumi zinakuwa kisingizio tu.
  Kujitoa kwa Chad ni hasara kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilioingia gharama za maandalizi ya mchezo wa marudiano, ikiwemo kuandaa tiketi za mchezo.
  Kama Chad wangekuwa na majibu ya mapema japo baada ya mchezo wa kwanza tu D’jamena, TFF isingeingia gharama za ziada na ingevunja kambi, au ingeandaa mchezo wa kirafiki.
  Aidha, kujitoa kwa Chad kumewanyima nafasi Watanzania kumuona kwa mara ya kwanza mshambuliaji Abdillah Yussuf ‘Adi’ wa timu ya Daraja la Pili England, Mansfield Town aliyejiunga na kambi ya Taifa Stars kwa mara ya kwanza safari hii.

  Ndoto za mshambuliaji wa Mansfield Town ya Daraja la Pili England, Abdillah Yussuf ‘Adi’ kuichezea Taifa Stars kwa mara ya kwanza zimeyeyuka

  Wachezaji waliokuwa kambini Taifa Stars chini ya makocha Charles Boniface Mkwasa na Hemed Morocco kwa maandalizi ya mchezo huo ni makipa; Shaaban Kado, Aishi Manula na Ally Mustafa ‘Barthez’.
  Mabeki; Juma Abdul, Shomary Kapombe, Mwinyi Hajji, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni, Kevin Yondan na David Mwantika.
  Viungo; Ismail Khamis ‘Suma’, Said Ndemla, Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto, Himid Mao, Mohammed Ibrahim, Ibrahim Hajib, Deus Kaseke, Farid Mussa na Shiza Kichuya.
  Washambuliaji ni John Bocco, Thomas Ulimwengu, Nahodha Mbwana Samatta, Elias Maguri, Jeremiah Juma na Yussuf Adi. 
  Stars inashika nafasi ya tatu katika Kundi G, ikiwa na pointi nne baada ya kushinda mechi moja dhidi ya Chad, kufungwa na Misri 3-0 na kutoa sare ya 0-0 na Nigeria.
  Misri inaongoza Kundi hilo kwa pointi zake saba, ikifuatiwa na Nigeria yenye pointi tano. Misri na Nigeria wanarudiana Jumanne Cairo baada ya kutoa sare ya 1-1 Jumapili Kaduna.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: CHAD WAIKACHA TAIFA STARS, WAJITOA 'KIMOJA' AFCON Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top