• HABARI MPYA

  Alhamisi, Novemba 07, 2019

  ‘FYEKA FYEKA’ YAENDELEA YANGA SC, UONGOZI WAVUNJA NA KAMATI YA MASHINDANO PIA

  Na Saada Akida, DAR ES SALAAM
  KLABU ya Yanga SC imeendelea kufanyia marekebisho nafasi mbalimbali na leo imetangaza kuvunja Kamati ya Mashindano.
  Kamati ya Mashindano Yanga ilikuwa chini ya Mwenyekiti, Rodgers Gumbo, Makamu wake, Saad Mkhiji na wajumbe ni Hamad  Islam, Makaga, Leonard Bugomola, Ally Kamtande, Said Side, Bonnah Kamoli, Sudi Mlinda, Tom Lukuvi, Martin Mwampashi, Hamza Jabir Mahoka, Edward Urio, Kawina Konde, Abednego Ainea na Edwin Muhagama.
  Hatua hiyo inakuja siku mbili tu baada ya klabu kuvunja benchi zima la Ufundi liliokuwa chini ya Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambaye nafasi yake imekuchuliwa na kiungo na Nahodha wa zamani wa klabu hiyo, Charles Boniface Mkwasa ‘Master’.
  Kwa ujumla maamuzi haya yanafuatia Yanga SC kutolewa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho kufuatia kuchapwa 3-0 na wenyeji, Pyramids FC Jumapili Uwanja wa Jeshi la Anga wa Juni 30 mjini Cairo.
  Matokeo yaliifanya Yanga itolewe kwa jumla ya mabao 5-1 kufuatia kufungwa 2-1 kwenye mchezo wa kwanza mjini Mwanza wiki mbili zilizopita.

  Kocha mpya wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa (kushoto) akimpa maelekezo Msaidizi wake, Said Maulid ‘SMG’ mazoezini leo Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara 

  Zahera alijiunga na Yanga SC Mei mwaka jana akichukua nafasi ya Mzambia, George Lwandamina – na baada ya kuwa timu kwa miezi 15 bila kushinda taji lolote ameondolewa kwa pamoja na benchi lake zima la Ufundi.
  Aliyekuwa Msaidizi wake, Mzambia Noel Mwandila, Meneja Hafidh Saleh, Mtunza Vifaa, Mohamed Omar ‘Mpogolo’, Mchua Misuli, Jackob Onyango na Daktari Edward Bavu nao wanafuatana na bosi wao, wakati kipa wa makipa pekee Manyika Peter ndiye amependekezwa kubaki. 
  Katika kipindi cha miezi 15, Zahera ameiongoza Yanga katika jumla ya mechi 75 za kirafiki na mashindano, kati ya hizo akishinda 45, kufungwa 17 na sare 13.
  Msimu uliopita Yanga SC ilimaliza nafasi ya pili katika Ligi Kuu, nyuma ya Simba SC waliobuka mabingwa, wakati katika Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) ilitolewa katika Nusu Fainali na Lipuli FC ya Iringa.
  Msimu huu Yanga ilianzia katika Ligi ya Mabingwa Afrika na baada ya kuitoa Township Rollers ya Botswana kwa jumla ya mabao 2-1, ikitoa sare ya 1-1 Dar es Salaam na kushinda 1-0 Gaborone, ikaenda kutolewa na Zesco United ya Zambia kwa jumla ya mabao 3-2, ikitoka sare ya 1-1 nyumbani na kwenda kufungwa 2-1 Ndola.
  Ndipo ikaangukia kwenye kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika na baada ya kutolewa na Pyramids FC amepoteza ajira
  Katika Ligi Kuu hadi sasa msimu huu, Yanga SC imecheza mechi nne na kushinda mbili, sare moja  na kufungwa moja pia.  
  Tayari kikosi cha Yanga kipo mjini Mtwara chini ya Kocha Mkwasa anayesaidiwa na mchezaji mwingine wa zamani wa klabu, Said Maulid ‘SMG’ kuelekea mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kesho dhidi ya Ndanda FC Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: ‘FYEKA FYEKA’ YAENDELEA YANGA SC, UONGOZI WAVUNJA NA KAMATI YA MASHINDANO PIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top